Maambukizi Ya Sikio (Hali Mbaya ya Kuvimba Sehemu Ya Kati Ya Sikio)

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2024

Sikio la kati ni nafasi tupu nyuma ya kiwambo cha sikio lako. Sikio la kati lina mifupa 3 midogo ambayo hutuma mitetemo ya kiwambo cha sikio lako hadi kwenye neva za sikio la ndani.

Hali mbaya ya kuvimba sehemu ya kati ya sikio ni aina ya maambukizi ya sikio yenye maumivu, kwenye sikio lako la kati. Inatokea kwa ghafula na kwa kawaida hali inakuwa nzuri kwa haraka. Maambukizi yakidumu au yakijitokeza upya, yanaitwa maambukizi sugu ya sikio.

Ndani ya Sikio

Je, maambukizi ya sikio ni nini?

Sehemu mbalimbali za sikio lako zinaweza kupata maambukizi, lakini una uwezekano wa kupata maambukizi kwenye sikio lako la kati. Maambukizi kwenye sikio la kati pia huitwa kuvimba sehemu ya kati ya sikio Maambukizi ya sikio yanayotokea haraka na kupata unafuu haraka ni maambukizi makali ya sikio. Maambukizi ya sikio ambayo hayaishi au yenye kurejea kila mara ni maambukizi ya kudumu ya sikio.

  • Maambukizi ya sikio yanaweza kutokea katika umri wowote lakini yanatokea sana kwa watoto

  • Kwa kawaida huwa yanachochewa na mafua au mzio

  • Sikio lenye maambukizi linauma na huenda usiwezi kusikia vilevile

  • Maambukizi mengi ya sikio yanapata unafuu yenyewe, lakini madaktari wataandika dawa za kuua bakteria kwa maambukizi makali au kwa maambukizi ambayo hayataondoka yenyewe

Nini kinachosababisha maambukizi makali ya sikio?

Maambukizi makali ya sikio yanasababishwa na virusi au bakteria. Kuwa na mafua ya kawaida au mzio kunaweza kusababisha maambukizi ya sikio.

Maambukizi haya yanalijaza sikio la kati kwa kiowevu. Kukiwa na maambukizi ya bakteria, kiowevu hicho kinaweza kuwa usaha.

Dalili za maambukizi makali ya sikio ni zipi?

Dalili za kawaida ni:

  • Maumivu ya sikio

  • Kupoteza uwezo wa kusikia

Watoto wachanga wanaweza kuwa na harara au kupata shida kulala.

Watoto wadogo wanaweza kuvuta masikio yao, kuwa na homa, kuhisi kichefuchefu, kutapika au kuharisha.

Ikiwa maambukizi hayo yatasababisha tundu kwenye kiwambo cha sikio (kutoboka kwa kiwambo cha sikio), majimaji yanaweza kutoka kwenye sikio. Hali hii kwa kawaida inaondoa maumivu.

Matatizo ya maambukizi ya sikio ni yapi?

Watu wengi hawawi na matatizo. Watoto wanaopata sana maambukizi ya sikio wanaweza:

  • Kupoteza uwezo wa kusikia kwa muda mrefu

  • Tundu kwenye kiwambo cha sikio linaloendelea kutoa majimaji (maambukizi sugu ya sikio)

Kwa nadra sana, maambukizi ya bakteria yanaweza kuenea kwenda katika mfupa wa fuvu au kwenye ubongo.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina maambukizi ya sikio?

Madaktari watatumia tochi ya mkononi kujua ikiwa:

  • Kiwambo cha sikio lako kinavimba au ni chekundu

  • Kuna kiowevu nyuma ya kiwambo cha sikio lako

Je, madaktari wanatibu vipi maambukizi makali ya sikio?

Maambukizi makali mengi ya sikio yanaondoka bila matibabu, lakini madaktari wanaweza kukupa:

  • Dawa za kuua bakteria

  • Dawa ya maumivu kama vile acetaminophen au ibuprofen

  • Kwa watu wazima, wakati mwingine kinyunyizio cha kupunguza msongamano au vidonge

  • Kwa watu wenye mzio, vidonge vya antihistamini

Ikiwa maumivu ya sikio ni makali sana, madaktari huenda wakahitaji kutoa majimaji kwenye sikio lako la kati. Wanaweza kutengeneza tundu dogo kwenye kiwambo cha sikio ili kutoa majimaji au kuweka bomba kwenye kiwambo cha sikio ili majimaji yaendelee kutoka vizuri.

Ninawezaje kupunguza hatari kwa watoto wangu kupata maambukizi ya sikio?

  • Hakikisha watoto wako wanapata chanjo zao za utotoni

  • Usiache watoto wachanga wanywe kitu kwenye chupa wakiwa wamelala au kwenda kitandani na chupa

  • Usivitie sigara ndani au watoto wakiwepo