Ugonjwa wa Kuharisha Wakati wa Kusafiri

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2024

Je, ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri ni nini?

Ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri ni kuhara (kinyesi laini sana, cha majimaji) unachopata unaposafiri katika maeneo ya duniani ambapo maji yana vijidudu ndani yake kwa sababu hayajatibiwa (kuuliwa viini) ipasavyo. Katika maeneo haya, unaweza kuugua unapokunywa maji, kula chakula ambacho hakijapikwa, au kula chakula kilichooshwa au kutengenezwa kutumia maji.

Bakteria kama vile Escherichia coli (E. coli) katika maji ndio chanzo cha kawaida cha kuhara wakati wa kusafiri. Lakini virusi kama vile virusi vya noro (hasa kwenye meli za watalii) na bakteria nyingine, virusi, na vimelea pia vinaweza kusababisha.

  • Unaambukizwa ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri kutoka kwa bakteria, vimelea, au virusi vilivyo kwenye maji unayokunywa au kwenye chakula unachokula

  • Dalili kawaida huanza saa 12 hadi 72 baada ya kula chakula au kunywa maji yaliyoambukizwa na hudumu kwa siku 3 hadi 5

  • Kuna uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri unapotembelea nchi ambazo maji hayajauliwa viini vizuri

  • Ili kuzuia ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri, kunywa vinywaji vya chupa pekee, tumia maji ya chupa kupiga mswaki, na usitumie vipande vya barafu au kula matunda na mboga ambazo hazijapikwa

Nenda hospitalini ikiwa una homa au unahara kinyesi chenye damu.

Je, dalili za ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri ni zipi?

  • Kuhisi mgonjwa tumboni

  • Kuharisha

  • Kutapika

Ikiwa unatapika na kuhara sana, utakosa maji mwilini na kujihisi dhaifu.

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri?

Daktari atakuuliza kuhusu dalili zako. Madaktari huwa hawapimi ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri. Katika baadhi ya matukio, wanaweza kuchukua sampuli ya kinyesi (haja kubwa) chako ili kukifanyia vipimo vya kutafuta bakteria, virusi, au vimelea.

Je, madaktari hutibu vipi ugonjwa wa kuharisha kwa msafiri?

Daktari atakuambia:

  • Kunywa vinywaji kwa wingi

  • Wakati mwingine kunywa dawa ili kusitisha kuharisha kwako, kama vile loperamidi

  • Wakati mwingine kwa kutumuia dawa za kuua bakteria

Watoto walio chini ya umri wa miaka 2 na watu wazima walio na homa au wanahara kinyesi chenye damu hawapaswi kutumia dawa ya kusitisha kuhara.

Ikiwa utajisadia haja kubwa 3 au zaidi ambapo unaharisha kwa takribani saa 8, madaktari wanaweza kukupa dawa ya kuua bakteria.

Ikiwa vipimo vitapata kimelea kwenye kinyesi chako, madaktari watakupa dawa ya kutibu kimelea.

Je, ninawezaje kuzuia ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri?

  • Kula na kunywa katika mikahawa inayojulikana kuwa na chakula salama pekee—vyakula vinavyopikwa na kupakuliwa vikiwa moto kwa kawaida kuwa salama

  • Ikiwa unataka kula matunda, kula matunda ambalo unajimenyea mwenyewe pekee

  • Kunywa vinywaji vilivyo kwenye chupa au maji yaliyochemshwa pekee

  • Usile chakula kutoka kwa wachuuzi wa mitaani, bufee, na mikahawa ya vyakula vinavyopikwa au kuliwa kwa haraka

  • Usile saladi za mboga ambazo hazijapikwa au matunda au salsa iliyoachwa kwenye meza kwenye vyombo vilivyo wazi

  • Omba vinywaji bila vipande vya barafu, au hakikisha kuwa vipande vya barafu vimetengenezwa kwa maji ambayo yamechemshwa

  • Tumia maji ya chupa kupiga mswaki badala ya maji ya bomba ya eneo lako

Ikiwa una mfumo dhaifu wa kingamwili, daktari wako anaweza kukupatia dawa ya kuua bakteria ili kuzuia ugonjwa wa kuharisha wakati wa kusafiri.