Je! mikazo ya ghafula ya watoto wachanga ni nini?
Mikazo ya ghafula ya watoto wachanga ni aina ya kifafa katika watoto chini ya mwaka 1. Kifafa husababishwa na mlipuko usio wa kawaida wa shughuli za umeme kwenye ubongo.
Kila mkazo wa ghafula husababisha harakati ya kutetemeka ambayo hudumu kwa sekunde chache
Watoto wachanga wanaweza kuwa na mikazo mingi ya ghafla kwa mfululizo kwa dakika kadhaa na kisha wasiwe nayo kwa muda
Mikazo ya ghafla kwa kawaida huanza wakati watoto wako chini ya mwaka 1 na inaweza kuendelea hadi umri wa miaka 5
Watoto wengi ambao wana mikazo ya ghafla ya watoto wachanga wana tatizo kubwa la ubongo
Madaktari huangalia mawimbi ya ubongo ya mtoto kwa kutumia EEG (electroencephalogram) kutambua mikazo ya ghafla ya watoto
Madaktari humpa mtoto sindano na vidonge vya homoni kila siku, pamoja na vidonge vya kuzuia kifafa
Je, mikazo ya ghafula ya watoto inakuwaje?
Watoto walio na mikazo ya ghafula ya watoto wachanga kwa kawaida:
Hutetemeka mwili mzima
Huinua na kupinda mikono yao
Hupinda shingo na sehemu ya juu ya mwili mbele
Hunyoosha miguu yao
Kila mkazo wa ghafula hudumu kwa sekunde kadhaa. Kwa kawaida hutokea kwa vikundi, moja baada ya nyingine kwa muda wa dakika kadhaa. Kwa kawaida watoto wachanga hupata mikazo ya ghafula mara tu baada ya kuamka. Wakati mwingine wanapata mikazo ya ghafula wakati wanapolala.
Je, nini husababisha mikazo ya ghafula ya watoto wachanga?
Wakati mwingine sababu haijulikani. Lakini kwa kawaida mikazo ya ghafula ya watoto hutokea kwa watoto wachanga ambao wana tatizo kubwa la ubongo.
Watoto wenye matatizo ya ubongo ambayo husababisha mikazo ya ghafula kawaida hukua polepole kuliko watoto wengine. Kwa mfano, wanaweza kuchukua muda mrefu kusimama, kutembea, au kuelewa lugha. Baadaye wanaweza kuwa na matatizo ya kufikiri na kuwasiliana.
Je, madaktari watajuaje ikiwa mtoto wangu ana mikazo ya ghafula ya watoto wachanga?
Daktari wa mtoto wako anaweza kufanya kipimo kiitwacho EEG. Kipimo hiki hupima mawimbi ya ubongo. Madaktari wanaweza kutambua mikazo ya ghafula ya watoto kwa muundo wa wimbi la ubongo unaoonekana kwenye EEG.
Wakati wa kipimo hiki, vihisi vidogo huwekwa na vibandiko kwenye kichwa cha mtoto wako
Kipimo hiki hakina maumivu.
EEG inaweza kufanywa wakati mtoto wako yuko macho au amelala
Madaktari wanaweza pia kufanya vipimo kutafuta chanzo cha mkazo wa ghafula. Vipimo kama hivyo vinaweza kuwa:
Vipimo vya damu na mkojo
MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku, inayoonyesha picha za kina) za ubongo wa mtoto wako
Upimaji wa jenetiki
Je, matibabu ya mikazo ya ghafla ya watoto wachanga ni yapi?
Hakuna tiba ya mikazo ya ghafla ya watoto wachanga. Daktari wa mtoto wako atajaribu kupunguza idadi na nguvu ya mikazo ya ghafula kwa kumpa mtoto wako dawa, kama vile:
Homoni ya adrenokotikotropiki (ACTH) - sindano ya dawa ambayo mtoto wako atapata mara moja kwa siku
Kotikosteroidi za kumeza
Dawa za kusitisha mikazo ya ghafla
Ikiwa dawa za kila siku hazitasaidia kudhibiti mikazo ya ghafula ya mtoto wako, madaktari wanaweza kupendekeza upasuaji. Kwa upasuaji, madaktari huondoa sehemu ndogo ya ubongo inayosababisha mikazo ya ghafula ya mtoto wako. Ingawa upasuaji huo unaonekana kuwa wa kutisha, kwa kweli ubongo wa mtoto hupona haraka.