Hali ya Kukoma Kupumua kwa Njiti ni nini?
Hali ya kukoma kupumua kwa njiti ni pale ambapo mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati wake anapoacha kupumua kwa vipindi vifupi. Kukoma huku katika kupumua hudumu kwa sekunde 20 au zaidi na hutokea tena na tena.
Mara nyingi hali ya kukoma kupumua kwa njiti hutokea pale ambapo sehemu ya ubongo wa mtoto wako ambayo hudhibiti upumuaji inapokuwa haijakomaa
Kiasi cha mtoto 1 kati ya watoto 4 waliozaliwa kabla ya wakati wao hupata hali hii
Hali ya kukoma kupumua hutokea mara chache kwa wiki na miezi kadhaa wakati ubongo wa mtoto wako unakua
Anzisha tena upumuaji kwa kumgusa mtoto wako taratibu
Wakati mwingine madaktari hutumia kafeini, au mashine ya CPAP au chombo cha kupitisha hewa ili kusaidia kupumua
Je, nini husababisha hali ya kukoma kupumua kwa njiti?
Sababu za kukoma kupumua kwa njiti ni pamoja na:
Sehemu ya ubongo wa mtoto wako ambayo hudhibiti upumuaji inapokuwa haijakomaa
Koo au njia ya hewa ya mtoto wako aliyezaliwa kabla ya wakati wake imefungwa kwa muda kwa sababu ya misuli dhaifu ya ulimi au kujipinda kwa mbele katika shingo
Matatizo haya hupotea mtoto wako anapokua na ubongo na misuli kukomaa.
Zipi ni dalili za hali ya kukoma kupumua kwa njiti?
Dalili zinajumuisha:
Hali ya kukoma kupumua kwa mtoto wako ambayo hudumu kwa sekunde 20 au zaidi
Ngozi ya kibuluubuluu au iliyopauka
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtoto wangu ana hali ya kukoma kupumua kwa njiti?
Wewe na daktari wako mnaweza kuona kusitasita katika upumuaji. Pia mtoto wako anaweza kuvaa kifaa cha kufuatilia ambacho kitapiga kengele ikiwa ataacha kupumua.
Madaktari wanaweza kufanya vipimo ili wawe na uhakika kuwa kukoma kupumua hakusababishwi na tatizo jingine la kiafya. Huenda wakafanya:
Vipimo vya damu
Vipimo vya mkojo
Je, madaktari hutibu vipi hali ya kukoma kupumua kwa njiti?
Madaktari hutibu matatizo yoyote yanayosababisha kukoma kupumua.
Wakati wa kusitasita kupumua, madaktari watakuelekeza umguse mtoto wako kwa taratibu ili kusaidia kuanza tena kupumua.
Iwapo mtoto wako anakumbana na hali ya kukoma kupumua kila mara:
Mtoto wako anaweza kuhitaji kuwa katika NICU (kitengo cha wagonjwa mahututi kwa watoto wachanga)
Madaktari wanaweza kumpatia kafeini mtoto wako, ambayo huchochoea kupumua
Mtoto wako anaweza kuhitaji mashine ya CPAP (shinikizo la njia ya hewa endelevu) au chombo cha kupitisha hewa ili kusaidia kupumua
Kama walivyo watoto wengine, watoto wenye hali ya kukoma kupumua kwa njiti wanapaswa kulala chali na si kifudifudi. Daktari wako atakagua ili kuhakikisha kuwa mtoto wako anaweza kusafiri kwa kukaa kwenye kiti cha gari kwa usalama.