Uharibifu wa retina kwa mtoto mchanga aliyezaliwa kabla ya wakati wake (ROP) ni nini?
Uharibifu wa retina kwa mtoto mchanga aliyezaliwa kabla ya wakati wake (ROP) ni tatizo la macho kwa njiti (watoto waliowahi sana kuzaliwa kabla ya wakati). Unasababishwa na mishipa ya damu iliyo nyuma ya jicho inapokua katika hali isiyo ya kawaida.
ROP huwapata zaidi watoto ambao wamezaliwa kabla ya ujauzito kufikisha wiki 30, hasa watoto waliozaliwa kabla ya wakati wao ambao wana maambukizi, damu kuvuja kwenye ubongo, au matatizo ya mapafu
Watoto waliozaliwa kabla ya wakati wao wanapaswa kuchunguzwa na daktari wa macho kila baada ya wiki 1 hadi 3
Kwa kawaida ROP huwa ni tatizo dogo, lakini wakati mwingine inaweza kusababisha retina kuachia, hivyo kusababisha kupungua kwa uwezo wa kuona au upofu
Mtoto wako anaweza asihitaji matibabu yoyote, au madaktari wanaweza kutumia matibabu ya leza au upasuaji
Je, nini husababisha ROP?
Kwa kawaida, mishipa ya damu ndani ya retina ya kijusi huanza kukua wakati kijusi kikiwa na kiasi cha wiki 18 hadi 20. Mishipa hiyo ya damu huacha kukua wakati mtoto anapozaliwa. Kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati wao, mishipa ya damu inakuwa bado haijamaliza kukua wakati mtoto anapozaliwa. Inaweza kuacha kukua kwa kipindi kifupi, lakini ikaanza tena kukua tena katika namna isiyo na utaratibu. Hii husababisha ROP.
Dalili za ROP ni zipi?
Watoto wachanga wenye ROP kwa kawaida huwa hawana dalili zozote, hivyo basi watoto wote waliozaliwa kabla ya wakati wao wanapaswa kuchunguzwa macho kuona kama wana ROP.
Watoto wenye ROP kali wanaweza kuwa na:
Kuvuja damu kwenye vijishipa vya damu vya macho
Wakati mwingine, kuachia kwa retina na matatizo ya kuona
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtoto wangu ana ROP?
Ikiwa mtoto wako atazalilwa kabla ya kufikisha wiki 30 au akizaliwa na uzito wa chini ya pauni 3, madaktari watamchunguza macho kuona kama ana ROP. Madaktari watachunguza macho kila baada ya wiki 1 hadi 3 hadi pale mishipa ya damu kwenye macho ya mtoto wako itakapokua kikamilifu.
Je, madaktari wanatibu vipi ROP?
Wakati mwingine, ROP haihitaji matibabu. Ikiwa unahitaji matibabu, huenda daktari akafanya yafuatayo:
Wanatumia matibabu ya leza kuzuia ukuaji wa mishipa ya damu isiyo ya kawaida
Wanachoma dawa
Ikiwa retina ya mtoto wako itaachia, madaktari watafanya upasuaji wa kuipachika tena.