Maambukizi ya Njia ya Mkojo (UTI) kwa Watoto

Imepitiwa/Imerekebishwa Oct 2023

Njia ya mkojo hujumuisha:

  • Figo (viungo 2 vilivyo na umbo la maharagwe vinavyotengeneza mkojo)

  • Ureta (mirija 2 inayotoa mkojo kutoka kwenye kila figo hadi kwenye kibofu cha mkojo)

  • Kibofu cha mkojo (kiungo kinachofanana na puto kinachoshikilia mkojo hadi uwe tayari kukojoa [mkojo])

  • Urethra (mrija wa kupitisha mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo hadi nje ya mwili)

Njia ya Mkojo

Je, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) ni nini?

Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) ni maambukizi ya bakteria kwenye baadhi ya sehemu ya njia ya mkojo. Mahali penye maambukizi zaidi ni kibofu cha mkojo.

  • UTI husababishwa na vijidudu (bakteria)

  • Kwa watoto wachanga, homa inaweza kuwa dalili pekee ya UTI

  • Watoto wakubwa wanaweza kuhisi maumivu au hisia za kuchomwa wakati wa kukojoa na haja ya kukojoa mara kwa mara

  • Kuna uwezekano mkubwa wa wavulana wachanga kupata UTI kuliko wasichana wachanga, lakini wasichana wakubwa wana uwezekano mkubwa wa kupata UTI kuliko wavulana wakubwa

  • Madaktari hutibu UTI kwa kutumia dawa za kuua bakteria

Je, UTI husababishwa na nini?

UTI husababishwa na bakteria wanaoingia kwenye kibofu cha mkojo na figo. Kwa kawaida, bakteria kutoka kwenye ngozi huingia ndani ya mwili kupitia urethra (mrija unaopitisha mkojo nje ya mwili).

Kuna uwezekano mkubwa wa UTI kutokea ikiwa mtoto wako ana kasoro ya kuzaliwa kwenye njia ya mkojo. Kasoro za kuzaliwa mara nyingi huzuia mkojo kutoka kwa kawaida. Mkojo ambao hautiririki kawaida ni kama maji yaliyotuama na kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa. Ikiwa kasoro ya kuzaliwa haijatibiwa, matatizo makubwa ya figo yanaweza kutokea baadaye.

Watoto waliozaliwa hivi karibuni wanaweza kuugua sana ikiwa UTI itaenea kupitia damu hadi kwenye sehemu zingine za mwili (hii inaitwa sepsisi).

Je, dalili za UTI ni zipi?

Dalili hutofautiana kulingana na umri.

Kwa watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka 2, dalili zinaweza kujumuisha:

  • Homa

  • Kutapika

  • Kuharisha (kutokwa kinyesi chepesi cha majimaji na kinachotoka mara kwa mara)

  • Mkojo wenye harufu mbaya sana

Watoto waliozaliwa hivi karibuni walio na UTI wanaweza kuugua sana. Wanaweza kupata maambukizi makubwa ya mwili mzima yanayoitwa sepsisi.

Watoto walio na umri wa zaidi ya miaka 2 wana dalili tofauti kulingana na iwapo kibofu chao cha mkojo au figo zimeambukizwa.

Watoto walio na umri wa zaidi ya miaka 2 walio na maambukizi ya kibofu cha mkojo wanaweza kuwa na:

  • Maumivu au hisia ya kuchomwa wakati wa kukojoa

  • Haja ya kukojoa mara kwa mara na ghafla

  • Maumivu katika sehemu ya kibofu cha mkojo (katika tumbo la chini)

  • Mkojo wenye harufu mbaya sana

Watoto walio na umri wa zaidi ya miaka 2 walio na maambukizi ya figo wanaweza:

  • Kuwa na maumivu juu ya figo moja au zote mbili (upande au nyuma karibu na kiuno)

  • Homa kali na mzizimo

  • Kuhisi wagonjwa sana

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtoto wangu ana UTI?

Madaktari hufanya:

  • Vipimo vya mkojo (kupima mkojo) kutafuta seli nyeupe za damu na bakteria kwenye sampuli ya mkojo

  • Kipimo cha mkojo ili kutambua bakteria zozote ziliopo

  • Vipimo vya picha, kama vile uchunguzi wa picha unaotumia mawimbi ya sauti, ili kuangalia kibofu cha mkojo na figo za mtoto wako

Ili kupata sampuli ya mkojo kutoka kwa watoto wadogo na watoto wachanga, madaktari huingiza mrija laini na mwembamba (mrija wa catheta) kupitia urethra yao. Sampuli ya mkojo huletwa kwenye maabara ili kuona ikiwa mkojo huo una seli nyeupe za damu na bakteria. Mkojo huo utatumwa pia kwa vipimo ili kutambua aina ya bakteria na dawa za kuua bakteria.

Wakati mwingine daktari wako atafanya vipimo ili kuangalia kasoro ya kuzaliwa katika njia ya mkojo ya mtoto wako. Kwa kawaida madaktari hufanya vipimo hivyo ikiwa mtoto wako ana umri wa chini ya miaka 3. Wanaweza pia kufanya vipimo kama hivyo ikiwa mtoto wako ni mkubwa na amekuwa na UTI mara kadhaa au alikuwa mgonjwa sana.

Kipimo cha kwanza kwa kawaida ni kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti. Ikiwa kuna tatizo kwenye njia ya mkojo, madaktari wanaweza kufanya kipimo kiitwacho voiding cystourethrography, ambacho huchunguza uhusiano kati ya kibofu cha mkojo na figo. Madaktari hupitisha catheta kupitia kwa urethra ya mtoto wako hadi kwenye kibofu cha mkojo, kama vile wanavyokusanya mkojo. Kisha kioevu maalum kinachoonekana kwenye eksirei hutiwa kwenye kibofu cha mkojo kupitia katheta, na eksirei huchukuliwa kabla na baada ya mtoto wako kukojoa.

Je, madaktari wanatibu vipi UTI?

Madaktari hutibu UTI kwa kutumia dawa za kuua bakteria.

Wakati mwingine mtoto wako anaweza kuhitaji upasuaji ili kurekebisha tatizo, kama vile kasoro ya kuzaliwa ya njia ya mkojo.

Je, ninawezaje kumkinga mtoto wangu asipate UTI?

Baadhi ya njia za kusaidia kuzuia UTI ni pamoja na:

  • Wasichana wanashauriwa kupanguza kutoka mbele kwenda nyuma baada ya kutumia choo ili kuepuka kupata bakteria kwenye urethra

  • Usiwape watoto kioevu, fuwele, au poda iliyoongezwa kwa maji ya kuoga ili kufanya iwe na povu na kuwa na harufu nzuri, ambayo yanaweza kufanya iwe rahisi kwa bakteria kuingia kwenye urethra

  • Tibu tatizo la kufunga choo (shida ya kupitisha kinyesi kigumu) kwa sababu inaweza pia kufanya iwe ngumu kukojoa na hivyo kusababisha UTI

  • Zingatia tohara kwa wavulana wanaopata UTI mara kwa mara

Ikiwa mtoto wako ana kasoro ya kuzaliwa ya njia ya mkojo, wakati mwingine madaktari huagiza dozi ya kila siku ya dawa za kuua bakteria ili kuzuia UTI.