Ugonjwa wa Selimundu

Imepitiwa/Imerekebishwa Dec 2022

Ugonjwa wa selimundu ni nini?

Ugonjwa wa selimundu ni tatizo la muda mrefu kwenye seli nyekundu za damu yako. Ni kitu ulichozaliwa nacho ambacho kinasababisha baadhi ya seli nyekundu za damu yako kuwa na umbo lisilo la kawaida. Badala ya kuwa na umbo linalofanana na diski, zinakuwa na umbo kama la nusu mwezi (mwezi mwandamo).

Umbo la nusu mwezi la seli nyekundu za damu ni kwa sababu zinajumuisha umbo lisilo la kawaida la hemoglobini. Hemoglobini ni dutu iliyo kwenye seli nyekundu za damu ambayo inabeba oksijeni. Umbo la nusu mwezi linasababisha seli nyekundu za damu kuvunjika kwa urahisi na zisitoshee vizuri kwenye mishipa midogo ya damu ili kusafirisha oksijeni.

  • Ugonjwa wa selimundu unapatikana sana kwa watu wenye asili ya Afrika au Wamarekani Weusi

  • Ugonjwa wa selimundu unafanya seli nyekundu za damu yako kuvunjika kwa urahisi, na kusababisha kiwango cha chini cha damu (anemia)

  • Seli za damu zisizo za kawaida haziwezi kupita kwenye mishipa midogo ya damu, ikisababisha maumivu, ukuaji duni na hatimaye matatizo ya viungo kama vile figo na bandama lako.

  • Watu walio na ugonjwa wa selimundu wana uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi fulani

  • Madaktari wanabaini ugonjwa wa selimundu kwa kutumia kipimo cha damu

  • Matibabu yanalenga kupunguza dalili, lakini matibabu ya seli shina yanaweza kutibu kwa baadhi ya watu

Nini kinachosababisha ugonjwa wa selimundu?

Ugonjwa wa selimundu unasababishwa na vinasaba unavyorithi kutoka kwa wazazi wako. Upo miongoni mwa wanafamilia. Unahitaji vinasaba viwili vya selimundu, kimoja kutoka kwa kila mzazi, ndipo unaweza kupata ugonjwa wa selimundu.

Kinasaba cha selimundu ni nini?

Kinasaba cha selimundu ni pale ambapo unakuwa na nakala moja tu ya jeni ya selimundu. Ikiwa nakala nyingine ya jeni ipo kawaida, basi huna ugonjwa wa selimundu.

Ikiwa watu wawili wenye kinasaba cha selimundu wakapata watoto, nusu ya watoto wao watakuwa na kinasaba hicho, robo yao watakuwa na ugonjwa wa selimundu na robo nyingine watakuwa kawaida. Watu wenye ugonjwa wa selimundu (si tu kinasaba) mara nyingi wanakuwa hawawezi kupata watoto.

Matatizo yatokanayo na ugonjwa wa selimundu ni yapi?

Si seli nyekundu za damu zote zina umbo la nusu mwezi unapokuwa na ugonjwa wa selimundu. Kadiri unapokuwa na seli zenye umbo la nusu mwezi, ndivyo unakuwa na uwezekano zaidi wa kuwa na dalili na matatizo. Kiwango cha chini cha oksijeni na sababu nyinginezo zinafanya seli nyekundu za damu za damu yako kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na umbo la nusu mwezi.

Seli nyekundu za damu zisizo za kawaida zinavunjika kwa urahisi. Kuvunjika kunaweza kusababisha:

Seli nyekundu za damu zisizo za kawaida hazipiti kwenye mishipa midogo ya damu kwa urahisi, kwa hivyo viungo vya mwili havipati damu ya kutosha. Mtiririko wa damu unapozuiwa, dalili zako zinategemea ni sehemu gani za mwili zilizoathiriwa:

  • Mifupa: Maumivu (wakati wa maumivu makali), jeraha kwenye maungio ya nyonga

  • Ubongo: Kiharusi

  • Moyo: Moyo kutanuka na moyo kushindwa kufanya kazi

  • Figo: Figo kushindwa kufanya kazi, maumivu ya figo

  • Mapafu: Ugonjwa mkali wa kifua

  • Uume: Kuvimba kwa uume (kudinda kwa maumivu kwa muda mrefu)

  • Ngozi: Vidonda sugu vya ngozi

  • Bandama: Bandama lililosinyaa, ambalo huongeza hatari ya maambukizi fulani

Mdororo wa aplastiki ni wakati ambapo uboho wako unasita kwa ghafula kutengeneza seli nyekundu za damu mpya na hali yako ya anemia inakuwa mbaya zaidi kwa haraka sana.

Je, dalili za ugonjwa wa selimundu ni zipi?

Watu wenye ugonjwa wa selimundu wote wana:

  • Dalili za anemia (kujisikia dhaifu na kuchoka na kuonekana umesawijika)

Baadhi ya watu wana dalili kadhaa nyingine, wakati wengine wana dalili mbaya sana wakiwa na ulemavu mkubwa na kifo cha mapema.

Mgogoro wa selimundu

Mgogoro wa maumivu ya selimundu ni wakati ambapo baadhi ya sehemu za mwili wako hazipati oksijeni ya kutosha. Ishara na dalili za mgogoro wa maumivu hujumuisha:

  • Maumivu kwenye tumbo lako, mgongo au mifupa mirefu ya mikono na miguu yako

  • Homa

  • Kutapika

Mgogoro wa selimundu unaweza kusababishwa na kitu chochote ambacho kinapunguza kiwango cha oksijeni kwenye damu yako:

  • Mazoezi magumu

  • Kupanda mlima

  • Kupaa kwenye mwinuko mrefu bila kuwa na oksijeni ya kutosha

  • Ugonjwa

Ugonjwa mkali wa kifua ni tatizo jingine ambalo linaweza kutokea wakati wa mgogoro wa selimundu. Ugonjwa mkali wa kifua kwa kawaida unatokea kwa watoto na unaweza hatari sana. Dalili zinajumuisha:

  • Maumivu makali ya kifua

  • Matatizo ya kupumua kutokana na kiwango cha chini ya oksijeni kwenye damu

Madaktari wanaweza kujuaje kuwa nina ugonjwa wa selimundu?

Madaktari watakuambia una ugonjwa wa selimundu kutokana na:

  • Vipimo vya damu

Unaweza kuhitaji kufanya vipimo, kulingana na dalili zako.

Vipimo vya uchunguzi wa ugonjwa wa selimundu ni vipi?

Vipimo vya uchunguzi ni vipimo ambavyo madaktari wanawafanyia watu ambao hawana dalili. Madaktari mara nyingi wanafanyia uchunguzi wa vipimo vya damu kwa ajili ya ugonjwa wa selimundu kwa:

  • Wazazi, ndugu na dada wa watu wenye ugonjwa wa selimundu

  • Watoto wachanga mara tu baada ya kuzaliwa

Madaktari wanaweza pia kukufanyia vipimo wewe na mwenzi wako kabla hujazaa mtoto ili kuona kama umebeba sifa bainishi ya selimundu na kama unaweza kuirithisha (uchunguzi wa ubebaji).

Je, madaktari wanatibu vipi ugonjwa wa selimundu?

Madaktari wanatibu ugonjwa wa selimundu ili:

  • Kuzuia migogoro

  • Kudhibiti anemia

  • Kusaidia kupunguza dalili

Madaktari wanatibu ugonjwa wa selimundu kwa kutumia:

  • Dawa

  • Folate, vitamini ambayo inasaidia mwili kutengeneza seli nyekundu za damu mpya

Mgogoro wa selimundu kwa kawaida unahitaji kwenda kwenye kitengo cha dharura na unaweza kuhitaji kulazwa hospitalini. Kwenye kitengo cha dharura na hospitalini, madaktari wanaweza kukupa:

  • Kiowevu kwenye mshipa wake (IV)

  • Dawa ya maumivu

  • kuongezewa damu

  • Oksijeni

  • Matibabu ya dalili ambazo zinaweza kuwa zimesababishwa na mgogoro, kama vile maambukizi

Upandikizaji wa seli shina ni mchakato wa kitabibu ambao unaweza kutibu ugonjwa wa selimundu kwa baadhi ya watu lakini ni hatari sana kwa hivyo inatumiwa tu katika hali zinazohatarisha maisha. Matibabu ya seli shina au jeni huenda siku moja yakatibu ugonjwa wa selimundu kwa usalama.

Ninawezaje kuzuia mgogoro na matatizo ya selimundu?

Unapaswa:

  • Epuka shughuli zinazopunguza oksijeni kwenye mwili wako

  • Mwone daktari kwa ajili ya magonjwa yako yote, hata yale madogo

  • Pata chanjo

Mara nyingi madaktari huwafanya watoto wenye anemia inayotokana na selimundu watumie penisilini kuanzia miezi 4 hadi miaka 6 ili kusaidia kuzuia maambukizi ambayo yanaweza kusababisha mgogoro wa selimundu.

Ni wapi ninaweza kujifunza zaidi kuhusu ugonjwa wa selimundu?