Je, Ugonjwa wa Kidole Tumbo ni Nini?

Kidole tumbo chako ni tyubu ndogo yenye umbo la kidole inayopatikana mwishoni mwa utumbo wako mpana.

Ugonjwa wa kidole tumbo ni uvimbe unaosababisha kidole tumbo chako kuvimba na kupata maambukizi.

Ugonjwa wa kidole tumbo husababishwa wakati kitu, kama vile kipande kidogo cha kinyesi kigumu kimezuia kidole tumbo chako. Uzibaji huu husababisha maambukizi na kuvimba.

Ukiwa na ugonjwa wa kidole tumbo, huenda ukapata maumivu yanayoanza katika sehemu ya katikati ya eneo la tumbo la juu na kuhamia kwenye sehemu ya chini kulia kwenye tumbo yako. Maumivu hayo yatazidi taratibu kwa kipindi cha siku moja au mbili. Maumivu yataongezeka ukisogea au ukikohoa au mtu anapobonyeza sehemu yenye maumivu.

Huenda pia ukapata matatizo kama vile kupoteza hamu ya kula, kuhisi kichefuchefu na kutapika, na wakati mwingine homa ya nyuzi 100 hadi nyuzi 101 Farenhaiti (nyuzi 37.7 hadi nyuzi 38.3 selsiasi).

Ili kutibu ugonjwa wa kidole tumbo, madaktari hufanya upasuaji ili kuondoa kidole tumbo chako kwa kukata wazi sehemu ya tumbo au kufanya laparoskopi. Pia utapewa dawa za kuua bakteria kupitia kwenye mshipa (IV)

Ikiwa tayari kidole tumbo chako kimepasuka wakati wa upasuaji, utahitaji kukaa hospitalini ili upate majimaji na dawa za kuua bakteria kwa njia ya mshipa kwa muda mrefu zaidi.

Hakimiliki © 2023 Merck & Co., Inc., Rahway, NJ, USA na washirika wake. Haki zote zimehifadhiwa.