Je, maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo husababishwa na nini?

Maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo: Muhtasari

Sehemu ya mgongo wa chini huruhusu mwili wako kugeuka, kujipinda, na kupinda, na hutoa nguvu ya kusimama, kutembea, na kuinua vitu. Inahusika katika karibu kila aina ya mwendo, hivyo maumivu katika sehemu ya chini ya mgongo ni ya kawaida sana.

Maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo kwa kawaida husababishwa na kuinua vitu, kufanya mazoezi, kuanguka, au kuhusika katika ajali ya gari. Sababu ya kawaida ya maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo ni mkazo wa misuli. Kuimarisha tumbo lako, nyonga, na misuli ya mgongo kunaweza kusaidia kuzuia maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo.

Unaweza kutibu maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo kwa kuepuka shughuli zinazosababisha mkazo kwenye mgongo wako na kutumia barafu au joto kwenye mgongo wako, lakini mara nyingi maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo kwa kawaida hupona yenyewe.

Maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo bila sababu zilizo dhahiri au ishara za tahadhari zilizoorodheshwa hapa chini yanaweza kuhitaji kumwona daktari.

Ni wakati gani sahihi wa kumwona daktari?

Muone daktari wako mara moja ikiwa una maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na ishara hizi za tahadhari:

  • Kufa Ganzi

  • Udhaifu katika mguu mmoja au yote miwili

  • Matatizo katika kukojoa au kupitisha kinyesi

  • Homa

  • Kuhisi wepesi kwenye kichwa au kuzirai

  • Maumivu makali popote kwenye tumbo lako

Muone daktari wako ndani ya siku moja ikiwa una maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na ishara hizi za onyo:

  • Historia ya saratani

  • Kupungua uzani

  • Maumivu makali usiku

  • Una umri wa miaka 55 au zaidi na hakuna sababu iliyo dhahiri, kama vile jeraha, linalosababisha maumivu yako

Uko kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi kwa sababu ya dawa unazotumia, upasuaji au jeraha la hivi karibuni, matumizi ya dawa za kulevya au kwa sababu una VVU au UKIMWI

Ikiwa maumivu yako si makali na huna dalili za tahadhari, unaweza kusubiri siku kadhaa kabla ya kuona daktari.

Je, maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo husababishwa na nini?

Madaktari huenda wasiweze kujua kila mara kile kinachosababisha maumivu yako ya sehemu ya chini ya mgongo. Sababu ya kawaida zaidi ni mkazo wa misuli au kuteguka kwa kano. Hii inaweza kutokea kwa upande mmoja au pande zote mbili za mgongo wako. Maumivu yako yanazidi kuwa makali unapotembea na ahueni unapopumzika.

Sababu nyingine za kawaida ni pamoja na:

  • Kubanwa kwa neva (wakati kitu kinakandamiza neva), jambo ambalo linaweza kutokea kwa hali kama vile ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo au hali ya kutoka kwa diski kwenye mifupa ya uti wa mgongo

  • Kusinyaa kwa mfereji wa uti wa mgongo katika sehemu ya chini ya mgongo wako (mfereji wa uti wa mgongo, njia ya uti wa mgongo ambayo uti wa mgongo hupitia, inakuwa ndogo sana)

  • Spondylolisthesis, ambapo mfupa wa mgongo huteleza kwa mbele juu ya mfupa ule ulio chini yake

  • Maumivu ya mwili mzima yanaweza pia kuathiri sehemu ya chini ya mgongo

Diski ni tishu zenye sponji kati ya mifupa ya mgongo ambazo huruhusu mgongo wako kuinama. Diski inapochanwa au kubanwa, nyenzo zinazofanana na jeli zinaweza kuvimba na zinaweza kuweka shinikizo kwenye neva. Kukohoa au kupiga chafya kunaweza kufanya maumivu ya mkazo wa neva kuwa mabaya zaidi.

Kusinyaa kwa mfereji wa uti wa mgongo katika sehemu ya chini ya mgongo wako ni sababu ya kawaida ya maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo kwa wazee. Maumivu yako yanaweza kuwa mabaya zaidi ikiwa utainua kitu kizito kwa njia isiyo sahihi, una uzito mkubwa, umechoka sana, una mkao mbaya, au misuri ya mgongo, tumbo na nyonga haina nguvu.

Je, siatika ni nini?

Maumivu ya siatika ni maumivu yanayosababishwa na shinikizo kwenye neva ya siatiki. Neva ya siatiki ndiyo neva kubwa zaidi ya kwenye mgongo, inaanzia kwenye sehemu ya chini ya mgongo hadi nyuma ya mguu wako. Kawaida maumivu makali ya siatika huathiri upande mmoja tu. Unaweza kuhisi kuchomwa na pini na sindano, kutetemeka au kupoteza hisia katika sehemu ya mguu wako, au kuwa na uchungu au maumivu makali kutoka kwenye sehemu ya chini ya mgongo, kupitia makalio, hadi nyuma ya mguu wako, hadi magoti au mguuni mwako. Mkazo unaoendelea kwenye neva ni jambo hatari na linaweza kusababisha udhaifu na kufa ganzi wa muda mrefu kwenye mguu wako.

Nini kitatokea katika ziara ya kumwona daktari?

Daktari wako atakuuliza maswali kuhusu dalili zako na historia ya afya yako na kufanya uchunguzi wa kimwili. Katika hali fulani, daktari wako anaweza kukufanyia vipimo kama vile eksirei, MRI, uchanganuzi wa CT, au elektromaiografia na uchunguzi wa uwezo wa neva kupitisha umeme.

Je, madaktari hutibu vipi maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo?

Madaktari hukita matibabu kulingana na sababu ya maumivu yako ya sehemu ya chini ya mgongo na muda ambao maumivu yamedumu. Lakini, kwa ujumla, maumivu mengi ya sehemu ya chini ya mgongo huisha baada ya huduma nzuri za nyumbani:

  • Ikiwa maumivu yako ni makali, unaweza kuhitaji kupumzika kwa siku moja au mbili.

  • Kupumzika sana sio kuzuri kwa sababu kunadhoofisha misuli yako ya mgongo, jambo ambalo linaweza kufanya maumivu yako kuwa mabaya zaidi.

  • Shughuli nyepesi kawaida husaidia. Uliza daktari wako nini unapaswa kufanya na kutofanya.

  • Weka joto au baridi kwenye eneo lenye maumivu. Baridi inafaa kwa siku mbili za kwanza baada ya jeraha. Kisha tumia joto.

  • Unapolala chini, unaweza kujihisi vizuri zaidi ukilala kwa upande huku magoti yakiwa yamekunjwa.

Haraka iwezekanavyo, daktari wako atahakikisha umeanza kufanya mazoezi mepesi ili kuimarisha mgongo wako. Unaweza kupelekwa ukafanye tiba ya kimwili ili kujifunza jinsi ya kufanya mazoezi ya mgongo na jinsi ya kuinua vitu na kusogea kwa usahihi.

Ikiwa madaktari wana uhakika kuwa maumivu hayatokani na mkazo wa neva au ugonjwa wa kudhoofika kwa viungo, unaweza kujaribu masaji au matibabu na tabibu maungo. Kwa maumivu ya muda mrefu, madaktari wanaweza kupendekeza kupunguza uzani, kichocheo cha neva cha umeme unaopitishwa kwenye ngozi, matibabu ya umeme ya nyumbani ambayo hukupa hisia za utulivu, za kusisimua, au upasuaji.

Kuna aina nyingi tofauti za upasuaji wa mgongo. Kwa kawaida, madaktari hupendekeza upasuaji tu wakati una dalili za mkazo mkali wa neva au ikiwa maumivu yako ni makali sana na hayapungui kwa matibabu mengine yote.

Je, ninawezaje kuzuia maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo?

  • Fanya mazoezi ya kunyoosha na kuimarisha misuli ya tumbo, nyonga na mgongo.

  • Hakikisha mgongo wako uko wima wakati umesimama na kuketi. Kukaa kwa mkao mbaya huleta mkazo kwa mgongo wako.

  • Keti huku miguu yako ikiwa kwenye sakafu, si miguu ikiwa imepishana.

  • Usisimame wala kuketi kwa muda mrefu.

  • Unaponyanyua vitu, nyanyua kwa miguu yako, si mgongo wako.

Hakimiliki © 2023 Merck & Co., Inc., Rahway, NJ, USA na washirika wake. Haki zote zimehifadhiwa.