Ugonjwa wa Selimundu

Ugonjwa wa selimundu unatokana na matatizo kwenye damu ambayo yanarithiwa kutoka kwa wazazi wote wawili. Hali hii hupata sana makundi fulani ya watu, kama vile Wamarekani wenye asili ya Afrika, Waarabu, Wagiriki, Waitaliano, Walatini na Wamarekani Asilia.

Seli nyekundu za damu za kawaida ni nyepesi sana na zina umbo la mviringo, zinafanana na donati. Wepesi na umbo lake huziruhusu kusafiri kwa uhuru kupitia katika mishipa midogo ya damu inayoitwa kapilari.

Kwa watu walio na ugonjwa wa selimundu, seli nyekundu za damu zinakuwa na umbo la nusu mwezi pia zinakuwa ngumu kujongea. Seli zisizo za kawaida zinakaa ndani ya kapilari, zikizuia mtiririko wa damu kwenda kwenye viungo muhimu.

Watu wenye anemia inayotokana na selimundu wanaweza kuwa na dalili kama vile macho na ngozi kuonekana kuwa na rangi ya manjano, ngozi iliyopauka, kukua taratibu, maumivu ya mifupa na viungo, kuongezeka hatari ya maambukizi, kuwa na vindonda vya ndani kwenye miguu, kuharibika jicho, anemia na uharibifu kwenye ogani zilizoathiriwa na uzuiaji.