Muhtasari wa Ugonjwa wa Lyme
Ugonjwa wa Lyme ni ugonjwa wa kuambukiza unaopatikana ulimwenguni kote. Nchini Marekani kwa kawaida husababishwa na bakteria wa Borrelia burgdorferi. Na aina zingine za hawa bakteria, Borrelia garinii na Borrelia afzelii, ni chanzo cha ugonjwa wa Lyme huko Ulaya na Asia. Na wengine wapya bado wanaendelea kugunduliwa. Ukweli ni kwamba, mwaka 2015 watafiti kutoka Mayo Clinic waligundua aina mpya ya bakteria inayosababisha ugonjwa wa Lyme na kuamua kuipatia jina la Borrelia mayonii.
Hivyo hawa bakteria wa Borrelia wote ni spirochete, na hii inamaanisha kwamba tofauti na walivyo bakteria wengine, hawa ni warefu, wembamba, wenye umbo la kujikunja na huzunguka au kujipinda ili kusogea.
Ugonjwa wa Lyme umewekwa katika kategoria ya zoonosis, maana yake ni kwamba huambukizwa kwa wanadamu kutoka kwa wanyama ambao wao ni hifadhi ya asili, hifadhi inamaanisha kuwa kwa kawaida bakteria hawa hawasababishi ugonjwa wowote mbaya kwa wanyama. Na spishi ya Borrelia inaweza kuambukizwa kwa wanyama mbalimbali, ikijumuisha wanyama wadogo kama panya, mijusi na ndege.
Bakteria hawa hawajulikani kwamba wanaweza kuambukizwa moja kwa moja kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu, lakini inasemekana kwamba wanahitaji vekta, maana yake aina fulani ya kiumbe cha kati ambacho kitawaeneza kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu.
Kutegemea na eneo, kuna vekta mbalimbali. Kwa mfano, kaskazini mashariki mwa Marekani, huenezwa kupitia Iksodes skapularis, kwa kawaida hujulikana kama kupe kulungu mwenye miguu myeusi. Lakini aina zingine za kupe wa Iksodes husambaza Borrelia ya Lyme huko magharibi mwa Amerika ya Kaskazini na Urasia, kama vile kupe wa kondoo, kupe wa taiga, na kupe wa mashariki mwenye miguu myeusi.
Sasa, kupe wanahitaji damu ili kuendelea kuishi. Na simaanishi kuwa tayari wana damu. Wanahitaji damu kutoka kwa kimelea au mlo wa damu, kama ilivyo kwa mbu, ruba, popo wanyonya damu, na viumbe vingine visivyopendeza sana. Ni wazi hali ya kuwa wanyonyaji damu, inawafanya kuwa wahusika dhahiri wa kueneza magonjwa yanayotokana na damu, sivyo? Na kupe wanahitaji kupitia hatua za kimaisha: buu, pupa, na kupe kamili. Hakuna utofauti mkubwa na sisi: Watoto, vijana, na watu wazima.
Kupe aliye katika hatua ya buu ana uwezekano mkubwa wa kupata bakteria wakati akila kupitia kitu kama panya, kwa sababu kupe wa kulungu wanapokuwa katika hatua za buu hupendelea wanyama wadogo. Baada ya hatua ya buu, kupe wa kulungu hunyonyoka na kuingia hatua ya pupa, na hula kupitia wanyama mbalimbali, maana yake ni kwamba wanaweza kusambaza bakteria waliowapata kwa hifadhi mpya. Baada ya kunyonyoka tena na kuingia katika hatua ya kukomaa, huzingatia sana kulungu, ambacho si kimelea kizuri sana kwa Borrelia. Hivyo, kwa kuwa kupe wa kulungu walio kwenye hatua ya buu na pupa husambaza Borrelia kwa vimelea vinavyofaa zaidi, hatua hizi mbili ni muhimu sana kwa Borrelia.
Sasa, kupe wa kulungu walio katika ahtua ya buu na kupe, japokuwa hiki si chakula chao pendwa, mara kwa mara hupata mlo kutoka kwa binadamu asiye na taarifa. Kama umewahi kuwa na kupe mwilini mwako, bila shaka utakubaliana nasi kwamba jambo la kwanza ambalo ungependa kufanya ni kumwondoa. Sehemu ngumu kuhusiana na kupe wa kulungu, hasa kupe wa kulungu ambao wako katika hatua ya pupa, ni kwamba ni wadogo sana, hivyo wakati mwingine ni vigumu kuwaona. Hii inamaanisha kwamba wanaweza kuruhusiwa kuendelea kula kwa muda mrefu, jambo ambalo linawaruhusu kupe kusambaza ugonjwa. Bakteria wa Borrelia husambazwa ndani ya mate ya kupe wakati akila, na kwa kawaida huchukua takribani saa 36 hadi 48 toka bakteria ajipachike kwa kupe kuweza kuhama kutoka kwenye utumbo wa kupe hadi kwenye mate yake na kisha kuingia kwa binadamu.
Iwapo Borrelia huambukiza mwanadamu, husababisha magonjwa katika hatua tatu. Kwa kawaida, hatua ya awali ya ugonjwa wa Lyme katika eneo dogo ni siku hadi wiki kadhaa tangu maambukizi ya kwanza. Bakteria wanavyosambaa kutoka eneo la mwanzo, wekundu na uvimbe husambaa pia. Wakati mwingine nafasi iliyopo kati ya sehemu iliyong'atwa mara ya kwanza na nusu kipenyo cha nje cha upele huwa haina bakteria, hivyo kusababisa upele wenye umbo la jicho la fahali, ambao pia hujulikana kama erithema migran, ambayo ni dalili ya mapema ya ugonjwa wa Lyme. Zaidi ya hayo, kunaweza kuwepo dalili za mafua yasiyo dhahiri wakati wa hatua hii pia.
Inayofuata ni hatua ya mapema ya uenezaji, ambayo kwa kawaida ni wiki hadi miezi kadhaa baadaye, wakati bakteria huanza kuenea kupitia mtiririko wa damu, au kuenea mahali kama moyo, ubongo, na viungo. Kwa ujumla, kwa kweli bakteria wachache ndio huvamia tishu hizi mbalimbali, lakini kwa kawaida mwitikio wa kingamwili huwa mkali sana, na hugeuza tishu hizi kuwa eneo la vita, kimsingi kwa kuua bakteria lakini uharibu tishu katika mchakato huu.
Hali zingine za erithema migran zinaweza kuanza kutokea katika maeneo ambayo hayana uhusiano na mahali palipong'atwa mwanzo. Na huu ndio wakati ugonjwa wa Lyme unapoweza kuwa mbaya sana. Pale bakteria wanapoambukiza tishu za moyo, hali hii hujulikana kama kadaitisi. Japokuwa kuvimba kwa tishu za moyo kunaweza kuathiri kila aina ya utenda kazi wa moyo, mara nyingi kitabibu hujidhihirisha kama kizuizi cha moyo cha AV, ikimaanisha kwamba mawimbi ya umeme yanayotoka chemba za juu hadi chemba za chini hushikiliwa, au kuzuiwa, hali ambayo hubadilisha muda wa mapigo ya moyo.
Pia ugonjwa wa Lyme unajulikana kuwa husababisha uvimbe kuzunguka neva ambazo zinadhibiti misuli ya uso, kimsingi kwa kubana neva na kusababisha kupooza kwa neva za uso, ambapo misuli ya uso huwa dhaifu au hata kupooza, hali ambayo inaweza kufanya iwe vigumu kutabasamu au kufunga macho. Kwa ugonjwa wa Lyme, mara nyingi hali hii ina pande mbili, maana yake ni kwamba hutokea pande zote mbili za uso.
Kama ugonjwa utasambaa hadi kwenye viungo, unaweza kusababisha ugonjwa wa baridi yabisi katika goti, kifundo cha mkono, na tindi ya mguu. Ugonjwa wa Lyme pia unaweza kusambaa hadi kwenye meninge, ambao ni utando wa uti wa mgongo na ubongo, hali ambayo husababisha homa ya uti wa mgongo na wakati mwingine shingo kukaza sana na maumivu ya kichwa.
Haishagazi kuwa, mwako katika viungo mbalimbali vya mwili unaweza pia kusababisha homa, uchovu, na dalili zingine zinazofanana na mafua, kama ambavyo tuliona katika hatua ya mwanzo ya maambukizi ya sehemu ndogo.
Ikiwa ugonjwa utaachwa usambae zaidi hadi kufikia hatua ya mwisho ya kusambaa, ambapo kwa ujumla inaweza kuchukua hadi mwaka mmoja tangu kutokea kwa maambukizi, dalili kuu ni ugonjwa sugu wa baridi yabisi katika kiungo kimoja au viungo vichache, ambapo mara nyingi hujumuisha goti.
Sasa utambuzi wa ugonjwa wa Lyme kwa kawaida hufanyika kwa kutazama kingamwili zinazopambana na protini za Borrelia. Jambo gumu ni kwamba wakati mwingine kingamwili huingiliana. Kwa maneno mengine ni kwamba, kingamwili ambayo iliundwa kwa ajli ya bakteria ya kawaida anayeishi kwenye utumbo inaweza kuingiliana ghafla na protini ya Borrelia kwa sababu zinafanana.
Ili kutofautisha mwenye Borrelia na asiyekuwa nayo, kuna vigezo vya ni aina ngapi za kingamwili mtu anazohitaji kuwa nazo ili kufanya utambuzi wa ugonjwa huo mahususi na kuondoa kile kinachoweza kuzingatiwa kama utambuzi usio wa kweli.
Ili kutibu ugonjwa wa Lyme, dawa za kuua bakteria ndilo chaguo la kwanza la matibabu, na zikitolewa katika hatua za mwanzo za ugonjwa, zina ufanisi mkubwa katika kuondoa bakteria, ingawa dawa maalum ya kuua bakteria inayotolewa mara nyingi inategemea mambo kama hatua ya ugonjwa na umri wa mgonjwa.
Pia ni jambo la muhimu kuwafuatilia wagonjwa wanaotibiwa kwa dawa za kuua bakteria kwa sababu wanaweza kupata athari za Jarisch-Herxheimer, ambapo hupata homa, kutokwa jasho, na misuli kuuma kwa athari za spirochete kupasuka na kuachia antijeni nyingi kwa wakati mmoja, hali ambayo huchochea sana kingamwili.
Mwishowe, mara baada ya wagonjwa kutibiwa ugonjwa wa Lyme, hali zao hupata nafuu sana. Kunaweza kuwepo wiki au miezi michache ambapo dalili za uchovu na maumivu ya misuli na vifundo huendelea, hali ambayo ni ya kawaida, lakini hali hii hupotea na haihusiani kabisa na kuendelea kuwepo kwa Borrelia mwilini. Kwa kweli, hakuna ushahidi kwamba bakteria huishi kwa muda mrefu katika mwili baada ya matibabu, na hakuna sababu ya kutumia dozi za muda mrefu za dawa za kuua bakteria au dawa nyingine kutibu ugonjwa wa Lyme.
Katika kuzuia, watu ambao hufanya kazi au kutembelea maeneo yenye miti mingi au maeneo yenye vichaka, uchafu wa majani ya miti na majani marefu wana hatari kubwa ya kupata kupe wa kulungu na kupata maambukuzi ya ugonjwa wa Lyme. Baada ya kusema hilo, kuchukua hatua za kuzuia ni muhimu kwa kila mtu kama vile kuvaa kofia na mashati ya mikono mirefu, pamoja na kutumia kinyunyuzio cha wadudu katika maeneo ambayo yanafahamika kwa kusambaza ugonjwa wa Lyme.
Ugonjwa wa Lyme (https://www.youtube.com/watch?v=rOQvpcpxbCs) kwa Mfyonzo (https://open.osmosis.org/) una leseni chini ya CC-BY-SA 4.0 (https://creativecommons.org/licenses/by-sa/4.0/).