
Haipalipidemia
Lehemu ni aina ya mafuta—kipengele muhimu kilicho katika seli zote za binadamu. Hata hivyo, mafuta au vitu vingine vya mafuta vinapozidi katika damu vinaweza kusababisha haipalipidemia na matatizo mengine ya mafuta. Haipalipidemia ni sababu ya msingi ya kutokea kwa atherosklerosisi na ugonjwa wa moyo.
Mfumo wa moyo na mishipa unajumuisha moyo, mishipa ya damu, na damu. Damu ina majukumu mengi ya kudumisha uhai, ikikumuisha kusafirisha oksijeni, kaboni dioksidi, virutubisho, na homoni katika mwili wote. Damu ina seli nyekundu za damu, seli nyeupe za damu, vigandishadamu, na virutubisho. Lehemu pia huzunguka kwenye mtiririko wa damu.
Aina mbili za lehemu zinazojulikana ni LDL, inayojulikana kama "lehemu mbaya" na HDL, inayojulikana kama "lehemu nzuri." Haipalipidemia ni neno linalotumiwa wakati damu ina kiwango cha juu cha LDL kuliko inavyopendekezwa.
Lehemu na vitu vingine vya mafuta huchanganyika katika mtiririko wa damu na huwekwa kwenye mishipa ya damu na kutengeneza utando fulani. Kuongezeka kwa mafuta kunaweza kusababisha utando kukua kwa muda, na kusababisha vikwazo katika mtiririko wa damu. Ikiwa kizuizi kinatokea kwenye mishipa ya moyo, kinaweza kusababisha shambulio la moyo. Na, ikiwa kizuizi kitatokea kwenye mishipa ya ubongo, inaweza kusababisha kiharusi.
Visababishi vya haipalipidemia vinaweza kujumuisha urithi na dawa fulani. Hata hivyo, sababu kubwa zaidi ya hatari inayoweza kubadilishwa ni chakula; lishe duni ni ile iliyo na ulaji wa mafuta zaidi ya 40% ya jumla ya kalori, ulaji wa mafuta mazito zaidi ya 10% ya jumla ya kalori; na ulaji wa lehemu zaidi ya miligramu 300 kwa siku.
Hakuna dalili za haipalipidemia, kwa hivyo uchunguzi wa mara kwa mara wa lehemu na vipimo vya damu unapaswa kuwa sehemu ya uchunguzi wa kimwili. Daktari au mtaalamu wa afya anaweza kupendekeza njia za kuzuia haipalipidemia.