Muundo wa Kawaida wa Seli ya Neva
Seli ya neva (nyuroni) hujumuisha kiini kikubwa cha seli na nyuzi za neva— nyongeza moja iliyorefushwa (aksoni) kwa ajili ya kutuma vichocheo na kwa kawaida matawi mengi (dendraitisi) ya kupokea vichocheo. Vichocheo kutoka kwenye aksoni huvuka sinapsi (muungano uliopo baina ya seli 2 za neva) hadi kwa dendraiti ya seli nyingine.
Kila aksoni kubwa imezungukwa na oligodendrosaiti katika ubongo na uti wa mgongo na Seli za Schwann katika mfumo wa neva wa pembezoni. Utando wa seli hizi una mafuta (lipoprotini) yanayoitwa myelini. Utando umefungwa kwa kukaza kuzunguka aksoni, na kuunda ala yenye matabaka mengi. kifunika myelini kinafanana na mfuniko wa mpira, sawa na ule unaozunguka waya wa umeme. Vichocheo vya neva husafiri kwa haraka zaidi kwenye neva zenye vifunika myelini kuliko kwenye zile ambazo hazina.