Historia ya Miongozo ya MSD

Maudhui yalibadilishwa mwisho Aug 2023

Mnamo 1899, kampuni ya kutengeneza dawa ya Marekani Merck & Co., Inc., Rahway, NJ, USA ilichapisha kwa mara ya kwanza kitabu kidogo cha marejeleo cha madaktari na wafamasia kilichoitwa Manual of the Materia Medica. Kilikusudiwa kuwasaidia madaktari na wafamasia kwa kuwakumbusha madaktari kwamba “Kumbukumbu husaliti.” Kitabu hicho kifupi ambacho ni rahisi kutumia na changamano cha Mwongozo (kama kilivyojulikana baadaye) kilipendwa sana na wahusika wa huduma za matibabu na wengine waliohitaji marejeleo ya kimatibabu. Hata Albert Schweitzer alipeleka nakala barani Afrika mwaka wa 1913, na Admiral Byrd alipeleka nakala hadi Ncha ya Kusini katika mwaka wa 1929. 

Miaka ilivyosonga, kila toleo lililofuata la kitabu hicho lilikua kwa ukubwa na upeo, na hatimaye kuwa mojawapo ya rasilimali za matibabu zinazotumiwa zaidi duniani.  Kufikia miaka ya 1980, kitabu hicho kilitafsiriwa katika lugha zaidi ya kumi na mbili.

Mnamo 1990, tulianzisha Mwongozo wa Tiba ya Wazee. Kitabu hiki kwa upesi kilikuwa kitabu cha kiada kilichouzwa zaidi cha tiba ya wazee, kilichotoa maelezo maalumu na ya kina kuhusu kutunza wazee. Toleo la 3 lilichapishwa katika lugha tano. Mwongozo wa Afya na Kuzeeka, uliochapishwa mwaka wa 2004, uliendeleza kujitolea kwetu kwa elimu ya huduma za wazee, uliotoa taarifa kuhusu kuzeeka na maswala ya afya ya wazee kwa maneno yanayoeleweka na umma.

Mwaka wa 1997, Mwongozo wa Taarifa za Matibabu-Toleo la Nyumbani ulichapishwa. Katika kitabu hiki kilicholeta mageuzi kamili, wahariri walitafsiri taarifa changamano za matibabu katika Mwongozo kuwa kwa lugha ya kila siku, hivyo kuzalisha kitabu kinachoweza kufikiwa na watu ambao hawakuwa na shahada ya tiba. Kitabu hichokilisasishwa mnamo 2003 kuwa Toleo la Pili la Nyumbani, na mwaka wa 2009 kuwa Kitabu cha Mwongozo wa Afya ya Nyumbani.

Mnamo 1999, toleo la karne (ya 17) la Mwongozo lilichapishwa na matoleo ya kwanza ya kidijitali ya Miongozo yalitolewa mtandaoni bila malipo. Muda mfupi baadaye, Miongozo ilitolewa kama programu za vifaa vya mikononi ili kunufaika kutokana na maendeleo ya teknolojia na kukidhi vyema mahitaji ya taarifa ya wasomaji.

Miaka ilivyosonga, Miongozo ya kitaaluma na ya watumiaji imetafsiriwa katika lugha 13. Baadhi ya tafsiri hizi pia zimefanywa ziwe zinapatikana mtandaoni.  Matoleo ya kidijitali ya Miongozo nje ya Marekani Kaskazini huitwa Miongozo ya MSD.

Mnamo 2014, uamuzi ulifanywa wa kuhamia kwenda machapisho ya kidijitali pekee. Kusasisha maudhui kidijitali mara kwa mara huruhusu Miongozo kuendana na maendeleo ya sasa ya haraka ya taarifa za matibabu. Uchapishaji wa kidijitali pia huruhusu Miongozo kujumuisha aina zote za midia anuwai na kuondoa hitaji la kuhakikisha taarifa zinatosha ndani ya mipaka ya upeo wa vitabu.