Je, chawa ni nini?

Chawa ni wadudu wadogo wanaokaa kwenye mwili wako au kwenye nguo na matandiko yako. Kuna aina 3 za chawa: kichwani, mwilini na kwenye sehemu za siri.

  • Chawa wanaenea kwa kuwa karibu sana na watu ambao wana chawa kwenye ngozi zao au kwenye vitu vyao vya binafsi, kama vile nguo au matandiko

  • Dalili kubwa inayosababishwa na chawa ni washo mkali

  • Madaktari watagundua kwamba ni chawa wanapowaona au mayai yao kwenye nywele zako.

  • Madaktari kwa kawaida wanwatibu chawa kwa kutumia shampuu maalumu, krimu au losheni na kukuambia usafishe nguo na matandiko yako

Kuangalia Chawa kwa Karibu

Aina tatu za chawa zinakaa kwenye mwili. .Chawa ana urefu wa hadi inchi 1/8 (milimita 3) kwa urefu.

Chawa wa kichwani

  • Chawa wa kichwani wanaishi kwenye nywele zako na kwenye ngozi ya kichwa chako—unaweza kuwaona na mayai yao (huitwa mayai ya chawa) kwenye kichwa chako

  • Wanaweza kuenea kwa urahisi kutoka kwa mtu moja kwenda kwa mwingine, hasa ikiwa unatumia pamoja brashi, kofia na vitu vingine

  • Chawa wa kichwani wanapatikana sana kwa wasichana wenye umri wa miaka 5 hadi 11, lakini mtu yeyote anaweza kuwapata

  • Kuwa msafi hakuwezi kuzuia kupata chawa wa kichwani

  • Dalili kubwa ni ngozi ya kichwa inayowasha

Chawa wa mwilini

  • Chawa wa mwilini wanaishi kwenye nguo na matandiko yako, si kwenye mwili wako, lakini wanatambaa na kuingia kwenye ngozi yako na kukuuma na kula damu yako

  • Wanapatikana sana kwa watu wanaoishi kwenye sehemu zenye msongamano au chafu

  • Wanaenea pale ambapo watu wanashiriki matandiko na nguo zenye chawa

  • Huwezi kuambukizwa chawa wa kwenye mwili kutoka kwa wanyama vipenzi wako

  • Tofauti na chawa wa kichwani, chawa wa kwenye mwili wanaweza kueneza ugonjwa fulani, kama vile homa kali iletwayo na chawa

Chawa wa kwenye sehemu za siri

  • Chawa wa kwenye sehemu za siri wanaishi kwenye sehemu zako za siri lakini pia wanaweza kuishi kwenye nywele za kifua chako, mapaja au uso.

  • Chawa wa kwenye sehemu za siri kwa kawaida wanaitwa kaa

  • Kwa kawaida wanaenea wakati wa kufanya ngono, lakini wanaweza pia kuenea wa kushiriki mataulo, matandiko au nguo.

  • Watoto wanaweza kupata aina hii ya chawa kwa kuwa karibu na mtu mzima mwenye chawa wa sehemu za siri

Dalili za chawa ni zipi?

Chawa kwa kawaida wanasababisha mwasho mkali.

Chawa wa kichwani ni vigumu kuwapata. Kwa kawaida ni rahi kuona mayai yao (mayai ya chawa). Mayai ya chawa yanajishikiza kwenye baadhi ya nywele zako karibu na shina la nywele. Unaweza kuwa na mayai machache au mengi sana.

Alama za kuumwa za chawa wa kwenye mwili zinaweza kusababisha vishimo vidogo vyekundu kwenye ngozi yako, kwa kawaida kwenye mabega yako, sehemu za siri na kwenye eneo la tumbo.

Alama za kuumwa za chawa wa kwenye sehemu za siri zinaweza kusababisha madoa ya rangi ya bluu kwenye sehemu zako za siri au sehemu nyingine walizouma. Chawa wa kwenye sehemu za siri kwa kawaida ni rahisi kuwapata kuliko chawa wa kichwani.

Je, madaktari wanawezaje kujua kuwa nina chawa?

Madaktari wanatambua kuwa una chawa kwa kuwatafuta au mayai yao (mayai ya chawa) kwenye mwili au nguo zako.

Kwa chawa wa kichwani, wanachana kwa uangalifu kwenye nywele zako zilizolowana ili kuwaona chawa walio hai. Kwa chawa wa kwenye sehemu za siri, wanaangalia tu nywele za sehemu zako za siri. Kwa chawa wa kwenye mwili, wanaangalia nguo zako, hasa kwenye upindo.

Madaktari wanatibu vipi chawa?

Madaktari wanatibu chawa kwa namna tofauti kutegemeana na aina gani ya chawa ulio nao. Lakini kwa aina zote za chawa, daktari wako atakuomba:

  • Kubadilisha, kufua au kusafisha kwa ukavu nguo zako na kufua matandiko yako kwenye maji ya moto kwa sabuni ya kufulia

  • Weka kitu chochote ambacho hakiwezi kufuliwa kwenye mifuko ya plastiki isiyopitisha hewa kwa wiki 2 ili kuua chawa

Matibabu ya chawa wa kichwani

  • Madaktari wanakutibu wewe na kila mtu kwenye familia yako ili kuondoa chawa wa kichwani kwa kutumia shampuu maalumu, krimu au losheni

  • Utaoaswa kutumia shampuu, krimu au losheni tena baada ya siku 7 hadi 10 ili kuua chawa yeyote ambaye alianguliwa tangu matibabu ya kwanza

  • Ikiwa matibabu haya hayatafanya kazi, madaktari wanaweza kukupa dawa kwa njia ya mdomo

Matibabu haya yanaua mayai ya chawa lakini hayayaondoi kwenye nywele zako. Ili kuondokana na mayai, unaweza kutumia kifaa maalumu cha kuchania nywele au uondoe moja moja kwa makini.

Madaktari hawana uhakika kama ni lazima kuwazuia watoto wenye chawa wa kichwani wasiende shuleni. Shule nyingi zina sheria zao kuhusiana na suala hili.

Matibabu ya chawa wa kwenye mwili

  • Madaktari wanatibu dalili zako, watakuambia ufue nguo zako na matandiko na kukuomba uwe msafi kadiri iwezekanavyo

Matibabu ya chawa wa kwenye sehemu za siri

  • Madaktari wanatibu chawa wa kwenye sehemu za siri kwa kutumia shampuu na krimu maalumu na wakati mwingine kwa kutumia dawa kwa kinywa

  • Mwenzi wako wa ngono atapaswa pia kupata matibabu

  • Kwa chawa walio kwenye kope zako, unaweza kutumia mafuta ya mgando kwa siku 8 hadi 10, tumia dawa fulani au dawa ya matone kwenye macho, au ondoa kwa makini chawa na mayai yake