Matibabu ya Ugonjwa wa Akili

Imepitiwa/Imerekebishwa May 2024

Je, madaktari huwashughulikia vipi wenye ugonjwa wa akili?

Matibabu makuu ni pamoja na:

  • Dawa

  • Tiba ya kuzungumza (tiba ya kisaikolojia au ushauri nasaha)

Kwa matatizo mengi ya afya ya akili, kutumia dawa pamoja na tiba ya mazungumzo ni bora zaidi kuliko kutumia moja pekee.

Matibabu mengine ni pamoja na:

  • Tiba ya mshtuko wa umeme

  • Uchangamshaji wa sumaku kupitia fuvu la kichwa (kuweka sumaku kichwani kwako ili kuchangamsha ubongo wako)

Je, ni dawa gani hutumika kwa ajili ya ugonjwa wa akili?

Madaktari hutumia dawa mbalimbali ili kutibu magonjwa ya afya ya akili. Aina za dawa zinazotumika ni pamoja na:

  • Dawa za kuzuia mfadhaiko, kama vile SSRI (vizuizi vya uchaguzi wa kuchukua tena serotonini)

  • Dawa ya kuzuia wasiwasi

  • Dawa za ukichaa

  • Viimarisha mihemko

Je, tiba ya kisaikolojia ni nini?

Katika tiba ya kisaikolojia, wakati mwingine huitwa tiba ya kuzungumza, madaktari na watoa ushauri huzungumza nawe kuhusu mawazo, hisia na tabia zako. Wanajaribu kutokuambia la kufikiria au kufanya. Badala yake, wanajaribu kukusaidia kujielewa na kutambua mbinu bora za kukabiliana na mfadhaiko na matatizo ya maisha. Tiba ya mtu binafsi inahusisha mtu mmoja anayeshughulikiwa na mtaalam mmoja wa matibabu. Pia mtaalam wa matibabu anaweza kutoa matibabu kwa kikundi, matibabu ya familia, au wanandoa

Mara nyingi wataalam wa matibabu wanatumia mbinu mbalimbali kutegemea tatizo. Baadhi ya aina za tiba ni pamoja na:

  • Tiba ya tabia

  • Tiba ya utambuzi

  • Tiba baina ya watu

  • Tiba nafsia

  • Tiba ya akili kwa mazungumzo

  • Tiba ya usaidizi wa kisaikolojia

Je, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni nini?

katika mshtuko wa umeme (ECT), madaktari hupiga ubongo wako mshtuko wa umeme wakati ukiwa katika hali ya unusukaputi.

  • ECT imeonyeshwa mara kwa mara kuwa na ufanisi kwa mfadhaiko mkali

  • Wakati mwingine unapoteza kumbukumbu kwa muda mfupi

Bila kujali jinsi ECT inavyoonekana kwenye vyombo vya habari, ECT ni salama na yenye ufanisi.

Je, ni aina gani ya madaktari hutibu magonjwa ya akili?

Aina mbalimbali za watoa huduma za afya hutibu magonjwa ya akili, na unaweza kuhudumiwa na timu ya watoa huduma, ikijumuisha:

  • Daktari wa magonjwa ya akili (daktari wa afya ambaye ana taaluma ya tiba ya magonjwa ya afya ya akili na anaweza kukuandikia dawa)

  • Mwanasaikolojia (Mweledi wa huduma ya afya ya akili anayetoa tiba)

  • Muuguzi

  • Mfanyakazi wa kijamii

  • Daktari wa huduma za msingi (anaweza pia kukuandikia dawa)