Anoreksia Nervosa

Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2024

Je, anoreksia nervosa (anoreksia) ni nini?

Anoreksia ni tatizo laa kula. Watu wenye anoreksia hupunguza ulaji wao wa chakula ingawa wanaendelea kupungua uzito. Wamejaa mawazo ya chakula na wanaweza kukataa kuwa wana shida. Ikiwa una anoreksia, unafanya mojawapo kati ya mambo haya mawili:

  • Kula chakula kidogo sana

  • Kula sana kwa wakati mmoja (kula kupindukia) kisha ujitapishe (kusafisha tumbo)

Matokeo yake ni kupoteza uzani zaidi kuliko inavyofaa kulingana na umri na ukubwa wako. Unaweza kupungua uzani hadi ukawa mgonjwa sana au hata kuaga dunia. Licha ya kuonekana mwembamba na mgonjwa, unaendelea kuamini kuwa wewe ni mnene sana.

Anoreksia inaweza kusababishwa na shinikizo la kijamii la kuwa mwembamba. Ugonjwa huu unaweza kuwa upo katika familia yako.

Je, dalili za anoreksia ni zipi?

Unapokuwa na anoreksia, maisha yako yote yanahusu kiasi cha chakula unachokula na uzani wako. Una hakika kuwa wewe ni mnene kiasi cha kutoweza kula chakula cha kutosha. Wakati mwingine unaweza kula kiasi kikubwa kwa mara moja na kisha ujitapishe. Hata unapozidi kuwa mwembamba sana, ungependa kuendelea kuwa mwembamba zaidi. Huenda yafuatayo yakatokea:

  • Unalalamika kuhusu kuwa na uzani mkubwa kupita kiasi, ingawa wewe ni mwembamba sana

  • Unafikiria kuhusu chakula kila wakati

  • Unapima chakula chako na kuhesabu kalori

  • Unakusanya, kuficha, au kutupa chakula chako

  • Unaruka milo

  • Kujifanya unakula au kusema uongo kuhusu kiasi gani ulichokula

  • Kufanya mazoezi mengi kuliko kawaida

  • Vaa nguo nyingi au kadhaa juu ya zingine

  • Kujipima uzani mara nyingi kwa siku

  • Kuhisi vizuri kujihusu kulingana na jinsi unavyofikiria kuwa unaonekana mwembamba

Je, tatizo la kukosa hamu ya chakula linaweza kusababisha matatizo gani?

Anoreksia sio tu kuonekana mwembamba sana. Ukipoteza uzani kupita kiasi, unaweza kuharibu mwili wako wote. Anoreksia inaweza kusababisha:

  • Kwa wanawake, hedhi yako kukoma

  • Kwa wanawake, nywele kukua usoni na mwilini mwako

  • Kuvimba au kujaa hewa tumboni

  • Maumivu ya tumbo

  • Kufunga choo (tatizo la kwenda haja kubwa)

  • Mfadhaiko

Ikiwa unajitapisha sana, asidi ya tumbo itaharibu meno yako. Anoreksia ikizidi kuwa mbaya sana, inaweza kuathiri uwiano wa kemikali mwilini mwako, jambo ambalo linaweza kusababisha kukonda kwa mifupa yako, matatizo makubwa ya moyo, au hata kifo.

Je, nani anaweza kupata anoreksia?

Mtu yeyote anaweza kupata anoreksia. Kuna uwezekano mkubwa wa kuanza katika miaka ya ujana au mwanzo wa utu uzima. Ni kawaida zaidi miongoni mwa wasichana na wanawake.

Watu wenye anoreksia mara nyingi wanaweza kuficha kutoka kwa wapendwa wao. Hii inamaanisha kuwa familia na marafiki huenda wasijue kuihusu hadi iwe mbaya sana na ya kuhatarisha maisha. Kuzifahamu dalili za anoreksia kunaweza kukusaidia kuitambua kwa mtu unayempenda.

Je, madaktari wanaweza kujuaje kama nina anoreksia?

Madaktari watachunguza urefu na uzani wako ili kuona ikiwa una uzani mdogo sana kwa jinsi ulivyo mrefu. Watakuuliza pia jinsi unavyohisi kuhusu mwili wako na uzani wako.

Ikiwa kuna uwezekano wa kuwa na anoreksia, madaktari watakufanyia vipimo vya kimwili. Wataagiza vipimo vya damu na mkojo ili kuchunguza matatizo yanayosababishwa na anoreksia. Kipimo cha kuchunguza ukonde wa mifupa yako na kipimo cha midundo isiyo ya kawaida ya moyo pia kinaweza kufanywa.

Je, madaktari hutibu anoreksia vipi?

Tiba ya kubadili tabia ya kula

Madaktari watakuomba umwone mtoa huduma wa afya ya akili kwa ajili ya matibabu. Tiba ya anoreksia:

  • Inajikita katika kujifunza tabia bora za kula na kufikia uzani bora kiafya

  • Inaweza kuwa ya mtu mmoja mmoja au ya kifamilia (tiba ya familia ni muhimu sana kwa vijana)

  • Inaweza kuendelea kwa hadi mwaka 1 baada ya kurejesha uzani

Tiba ya kurejesha uzani

Ikiwa umepoteza uzani mkubwa au kupoteza uzani haraka sana, madaktari watajaribu kukusaidia kurejesha uzani wako. Hii inaweza kuhusisha:

  • Kulazwa hospitalini ili kuhakikisha kuwa unakula vya kutosha

  • Uchunguzi wa mara kwa mara wa daktari

  • Kutembelea mtaalamu wa lishe (mhudumu wa afya anayehusika na ulaji bora)

Wakati mwingine madaktari hukupa dawa za kutibu wasiwasi na unyogovu. Wakati hisia zako ni bora, unaweza kula zaidi na kuongezeka uzani.