Prostatitisi

Imepitiwa/Imerekebishwa May 2023

Nyenzo za Mada

Je, tezi dume ni nini?

Tezi dume ni tezi inayopatikana kati ya kibofu cha mkojo na uume. Mrija wa mkojo (urethra) unaobeba mkojo kutoka kwenye kibofu hadi nje ya uume unapita katikati tezi kibofu.

Tezi dume hutengeneza majimaji ambayo hulinda shahawa. Karibu majimaji yote ambayo humtoka mwanaume wakati wa kujamiiana hutengenezwa na tezi dume.

Kwa vijana, tezi dume inatoshana na karanga lakini ukubwa wake huongezeka kadri unavyozidi umri.

Prostatitisi ni nini?

Prostatitisi ni uchungu na kuvimba kwenye tezi dume.

Prostatitisi husababishwa na nini?

Wakati mwingine, prostatitisi inasababishwa na maambukizi. Kwa kawaida maambukizi huenea kwenye tezi dume yako kutoka kwenye sehemu za mfumo wako wa mkojo (kama vile kibofu cha mkojo na mafigo). Nyakati zingine, prostatitisi haisababishwi na maambukizi lakini kisababishaji halisi si wazi.

Dalili za prostatitisi ni zipi?

Dalili za prostatitisi ni:

  • Uchungu kwenye sehemu ya chini ya mgongo, uume, pumbu au sehemu katikati mwa korodanina na tundu la haja kubwa (sehemu ya msamba)

  • Kuhitaji kukojoa (kutoa mkojo) mara nyingi na haja madhubuti ya kukojoa

  • Kuhisi maumivu au kuungua unapokojoa

  • Matatizo katika kupitisha kinyesi (mavi)

  • Uchungu wakati wa na ugumu wa kusimamisha uume au mshindo

Viungo vya uzazi vya mwanaume

Ikiwa bakteria ndio kisababishaji cha prostatitisi, kwa kawaida dalili huwa mbaya:

  • Homa, mzizimo, tatizo kukojoa na damu kwenye mkojo

  • Usaha kwenye tezi dume au viungo vyako vya ngono

Madaktari wanawezaje kujua kama nina prostatitisi?

Daktari wako atauliza kuhusu dalili zako, akwambie utoe sampuli za mkojo na afanye uchunguzi wa rektamu. Wakati wa uchunguzi wa rektamu:

  • Daktari huvalia glavu na kuingiza kidole kwenye rektamu yako (mwishoni mwa njia yako ya mmeng'enyo wa chakula ambapo kinyesi [haja kubwa] huhifadhiwa)

  • Daktari wako anaweza kuhisi tezi dume yako wakati wa uchunguzi

  • Ikiwa una prostatitisi, tezi dume yako itakuwa laini sana daktari wako akiiguza

Baada ya uchunguzi wa rektamu, utatoa sampuli nyingine ya mkojo. Daktari ataona kama mkojo una seli zaidi za usaha baada ya tezi dume yako kukandwa (kukanda tezi dume).

Madaktari hutibu prostatitisi vipi?

Madaktari hutibu prostatitisi tofauti ikiwa imesababishwa na bakteria au la.

Ikiwa bakteria ndizo visababishaji

  • Daktari wako atakupea dawa za kuua bakteria ambazo utatumia kwa angalau siku 30

  • Ikiwa uko mgonjwa sana, utahitaji kusalia hospitalini ili kupewa dawa za kuua bakteria kupitia kwenye mshipa wa damu

Ikiwa maambukizi yanarejea mara nyingi baada ya matibabu:

  • Daktari wako anaweza kukupea dawa za kuua bakteria ambazo utatumia kwa wiki 6

  • Unaweza kufanyiwa upasuaji ili kutoa usaha kwenye tezi dume yako

Ikiwa haukusababishwa na bakteria

Prostatitisi kwa kawaida huwa ngumu kutibu, lakini unaweza kutibu dalili kwa:

  • Kukanda tezi dume, ambayo daktari atafanya kwa kuweka kidole kwenye rektamu yako

  • Kuketi kwenye maji yenye joto

  • Mazoezi ya mwili na akili ili kusaidia misuli yako kutulia (mrejesho wa kibayolojia)

  • Dawa ambazo hufanya kupitisha kinyesi kuwe rahisi, hupunguza uchungu na kuvimba au hutuliza misuli yako ya tezi dume

Ikiwa dalili ni mbaya sana na matibabu mengine hayafanyi kazi, unaweza kuhitaji upasuaji ili kuondoa sehemu ya tezi dume.