Kiharusi cha joto

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Kiharusi cha joto ni nini?

Kiharusi cha joto ni hali ya dharura inayosababishwa na joto la mwili kupanda sana. Usipopunguza joto kwa haraka vya kutosha, unaweza kufariki au kuharibika kiungo au ubongo.

  • Kiharusi cha joto hutokea wakati uko na joto jingi sana na mwili wako unashindwa kupunguza joto wenyewe

  • Halijoto yako kwa kawaida huwa zaidi ya 104° F (40° C)

  • Kiharusi cha joto kinaweza kuathiri watu wakubwa au watoto wachanga ambao wanaishi bila kidhibiti joto

  • Wanariadha na watu wanaofanya kazi ngumu katika mazingira ya joto kali pia wako katika hatari ya kupata kiharusi cha joto

  • Kisipotibiwa, kiharusi cha joto kinaweza kuharibu ogani zako, kama vile ubongo, moyo na mapafu yako

  • Madaktari hupunguza joto la mwili wako na hukupea viowevu moja kwa moja kupitia kwenye mshipa wako (viowevu vya IV)

  • Bila matibabu, takribani asilimia 80 ya watu walio na kiharusi cha joto hufariki

Ita gari la wagonjwa mara moja ikiwa mtu ana dalili za kiharusi cha joto. Unaposubiri gari la wagonjwa, mtoe mtu huyo kwenye jua au joto. Mpunguzie joto mtu huyo kwa kumweka kwenye maji baridi, kama vile kwenye bahari, mto au hodhi. Ikiwa kupata maji baridi hakuwezekani, fanya ngozi ya mtu huyo iwe na unyevu kwa kutumia maji yenye joto kidogo na kupulizia hewa kwenye ngozi.

Kiharusi cha joto husababishwa na nini?

Unaweza kupata kiharusi cha joto kutoka kwa:

  • Kufanya kazi au mazoezi magumu wakati kuna joto

  • Kufungiwa kwenye gari lenye joto

  • Kuwa ndani ya chumba chenye joto kwa siku chache

Inaweza kuchukua tu saa chache za kufanya kazi au mazoezi kwenye joto ili kupata kiharusi cha joto, hasa ikiwa mwili wako haujazoea joto.

Watoto ambao wamefungiwa kwenye gari (au ambao ni wachanga sana kuweza kufungua mlango) kwenye jua kali wanaweza kupata kiharusi cha joto na kufariki chini ya saa moja. Magari yanapata joto jingi ndani kwa haraka, haswa kwenye jua.

Watu wazee ambao wamefungiwa kwenye chumba chenye joto kali katika msimu wa joto kwa siku chache wanaweza kupata kiharusi cha joto hata kama chumba hicho hakionekani kuwa na joto kali. Hatua kwa hatua mwili wao hulemewa na joto.

Dalili za kiharusi cha joto ni zipi?

Ukiwa unakuwa mgonjwa kutokana na jua, unaweza kosa kugundua kuwa halijoto ya mwili wako iko juu zaidi. Huenda ukaona dalili zifuatazo kama onyo la kiharusi cha joto:

  • Udhaifu, kizunguzungu na wepesi wa kichwa

  • Maumivu ya kichwa

  • Kuhisi mgonjwa kwenye tumbo lako au kutapika

Ikiwa una kiharusi cha joto, unaweza kutoa au kukosa kutoa jasho na:

  • Halijoto ya mwili wako inapanda zaidi ya 104° F (40° C)

  • Ngozi hukuwa joto, yenye uwekundu na wakati mwingine kavu

  • Ubongo huathiriwa na unakuwa mwenye kuchanganyikiwa, unaweza kuwa na mishtuko au unaweza kupata kifafa

Madaktari wanawezaje kujua kuwa nina kiharusi cha joto?

  • Madaktari wanaweza kujua kulingana na chenye kilikufanyikia, dalili zako na halijoto ya mwili wako

  • Watafanya vipimo vya damu na mkojo ili kuona kama viungo vyako vinafanya kazi vizuri

Madaktari hutibu vipi kiharusi cha joto?

Madaktari watakulaza hospitalini na wanaweza:

  • Kukutoa mavazi na kufunika ngozi yako na maji au barafu

  • Kutumia feni kupulizia hewa kwenye mwili wako

  • Kukupatia viowevu baridi kupitia kwenye mshipa

Ninawezaje kuzuia kiharusi cha joto?

Ili kuzuia kiharusi cha joto wakati kuna joto kali sana nje, ni muhimu:

  • Kuvaa mavazi mepesi ambayo hayabani sana

  • Kuepuka jua iwezekanavyo

  • Kunywa viowevu vingi hata kama hauhisi kiu

  • Kuepuka mazoezi ngumu katika nyakati joto zaidi za siku

  • Muulize daktari wako kama tatizo lolote ulilonalo au dawa ulizonazo zinaweza kuongeza hatari yako ya kupata kiharusi cha joto.

  • Kuangalia watu wazee, haswa wale ambao hawana vidhibiti joto

  • Kutowahi acha mtoto mchanga kwenye gari lililoegeshwa

Ikiwa unajua kuwa utafanya kazi au mazoezi kwenye joto, unapaswa kufanya mwili wako uzoee joto hio hatua kwa hatua. Usifanye kazi ya siku nzima au mazoezi makali mara moja.

  • Kwa zaidi ya takriban siku 10, ongeza hatua kwa hatua ugumu na muda ambao unafanya kazi kwenye joto

  • Katika mwisho wa muda huo, unapaswa kuwa unafanya shughuli kali za dakika 90 kwenye joto

Baada ya kufanya mazoezi haya, mwili wako utaweza vizuri kuhimili juhudi kwenye joto.

Kuwa sawa kimwili ni tofauti na kuzoea joto. Hata kama una afya nzuri, bado unapaswa kufuata hatua hizi ili kuweza kuzoea joto.