Maambukizi ya minyoo wa mchangouzi

(Enterobiasisi; Oksuriasisi)

Imepitiwa/Imerekebishwa Jul 2023

Je, maambukizi ya minyoo ya tumbo ni nini?

Minyoo ya tumbo ni vimelea ambavyo kwa kawaida huambukiza watoto, japokuwa watu wazima wanaweza kuambukizwa pia. Minyoo ya tumbo huishi kwenye utumbo na kutaga mayai yao kwenye ngozi inayozunguka tundu la haja kubwa (uwazi ambapo kinyesi (haja kubwa) hupita), na kusababisha mwasho.

  • Mwasho kwenye sehemu inayozunguka tundu la haja kubwa ni dalili ya minyoo ya tumbo

  • Watoto wanaonyonya vidole gumba wana hatari kubwa ya kupata minyoo ya tumbo kwa sababu wana nafasi kubwa ya kumeza mayai ya minyoo ya tumbo

  • Ikiwa unashuku kuwa mtoto wako ana minyoo ya tumbo, unaweza kufanikiwa kuona minyoo hiyo kwa kutazama sehemu ya tundu la haja kubwa la mwanao kwa kutumia tochi nyakazi za usiku—ni midogo, myeupe na imejinyonganyonga

  • Madaktari hutibu minyoo ya tumbo kwa dawa za kuzuia vimelea

Je, nini husababisha maambukizi ya minyoo ya tumbo?

Maambukizi ya minyoo ya tumbo husababishwa na minyoo wadogo ambao huingia kwenye utumbo.

  • Unapata maambukizi kwa kumeza mayai madogo ya minyoo ya tumbo

  • Mayai huanguliwa na kukua kwenye utumbo

  • Takribani wiki 2 hadi 6 baadaye, minyoo ya tumbo iliyokomaa hutoka nje ya tundu lako la haja kubwa na kutaga mayai yake madogo sana kwenye ngozi ya karibu

  • Unaweza kusambaza mayai hayo kwa watu wengine

Mayai hayo husababisha mwasho kwenye tundu lako la haja kubwa. Unapojikuna, unabeba mayai ya minyoo ya tumbo kwenye kucha zako na unaweza kuyasambaza kwa watu wengine. Mayai pia hufika kwenye mashuka yako na yanaweza kuathiri watu. Minyoo ya tumbo huwapata watoto zaidi kwa sababu huwa hawaoshi mikono kama wafanyavyo watu wazima.

Je, zipi ni dalili za maambukizi ya minyoo ya tumbo?

Watu wengi wenye minyoo ya tumbo huwa hawana dalili zozote: Iwapo una dalili, zinaweza kujumuisha:

  • Kuwashwa kwenye sehemu inayozunguka tundu la haja kubwa

  • Kwa wasichana, kuwashwa na harara kwenye sehemu inayozunguka uke

Je, madaktari wanawezaje kufahamu ikiwa nina maambukizi ya minyoo ya tumbo?

Iwapo madaktari wanafikiri kuwa mtoto wako anaweza kuwa na minyoo ya tumbo, kwa kawaida hukuomba utafute minyoo ya tumbo au mayai yake.

  • Kagua uwepo wa minyoo ya tumbo iliyokomaa kwenye sehemu inayozunguka tundu la haja kubwa la mtoto wako takribani saa 1 au 2 baada ya mtoto wako kusinzia—minyoo ya tumbo ni myeupe, iliyojinyonganyonga na myembamba kama unywele, lakini unaweza kuiona kwa macho yako.

  • Bandika kipande cha gundi kwenye sehemu inayozunguka tundu la haja kubwa la mtoto wako mara tu unapoamka asubuhi ili kunasa mayai yoyote—peleka kipande hicho cha gundi kwenye ofisi ya daktari wako ili akichunguze kwenye hadubini

Je, madaktari hutibu vipi maambukizi ya minyoo ya tumbo?

Madaktari hutibu maambukizi ya minyoo ya tumbo kwa:

  • Dawa za kuua vimelea—mara nyingi, hutumia dozi moja papo hapo, na dozi nyingine wiki 2 baadaye. 

  • Wakati mwingine, dawa za kuua vimelea kwa kila mtu kwenye familia yako ili minyoo ya tumbo isisambae

  • Malai ya kuzuia mwasho ya kupaka kwenye sehemu inayozunguka tundu la haja kubwa

Ili kuondoa mayai ya minyoo ya tumbo kwenye nyumba yako baada ya maambukizi:

  • Vuta vumbi kwa umakini katika nyumba yako yote

  • Osha kila kitu ambacho kimeguswa na mtu aliye na maambukizi, kama vile vitu vya kuchezea, mashuka, na nguo