Je, giardiasis ni nini?
Giardiasis ni maambukizi ya utumbo mdogo yanayosababishwa na kimelea kidogo sana kinachoitwa Giardia.
Unaweza kupata giardiasis kutokana na kunywa maji machafu
Wakati mwingine unapata giardiasis kutoka kwa watu wengine wenye maambukizi
Dalili kuu ni tumbo kukakamaa na kuharisha
Madaktari wanaweza kufahamu kwamba una maambukizi kwa kupima sampuli ya kinyesi (mavi)
Ili kuepuka giardiasis, chemsha maji yenye maambukizi kabla ya kuyanywa, hasa maji kutoka kwenye mkondo wa maji au mto
Madaktari hutibu giardiasis kwa dawa za kuua vimelea
Je, nini husababisha giardiasis?
Giardiasis husababishwa na vimelea wadogo wanaoitwa Giardia.
Giardia hupatikana zaidi kwenye maziwa, mito, na mikondo ya maji duniani kote. Pia wanaweza kuwa kwenye maji ambayo yanaonekana kuwa masafi na salama. Wakati mwingine, pia hupatikana kwenye maji ambayo hayakusafishwa vizuri kutoka kwa msambazaji wa maji ya jiji au mabwawa ya kuogelea.
Watu wengi hupata giardiasis kutoka kwenye maji ya kunywa ambayo ya vimelea ndani yake. Kwa sababu watu wenye giardiasis hupitisha vimelea kwenye kinyesi chao, wanaweza kusambaza maambukizi kwa bahati mbaya iwapo vitagusana na kitu ambacho utakiweka mdomoni mwako.
Je, dalili za giardiasis ni zipi?
Mara nyingi dalili huanza takribani wiki moja au mbili baada ya kupata maambukizi. Zinajumuisha:
Kukakamaa kwa tumbo
Kutoa gesi
Kuharisha kinyesi chenye majimaji, na harufu mbaya, hali ambayo inaweza kudumu kwa wiki kadhaa
Tumbo lako kuuma—hisia zinaweza kutokea na kupotea
Kuchoka na kujihisi vibaya na bila njaa
Kama kuhara kutadumu kwa kipindi kinachozidi wiki chache, hali hii inaweza kuzuia mwili wako kupata virutubishi unavyovihitaji. Unaweza kupungua uzani. Watoto ambao wanaendelea kuhara wanaweza kupata matatizo katika ukuaji wao.
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina giardiasis?
Madaktari watakuuliza kuhusu dalili zako na watafanya:
Vipimo vya kinyesi
Je, madaktari hutibu vipi giardiasis?
Daktari hutibu giardiasis kwa:
Dawa za kuzuia vimelea
Madaktari hutibu tu watu ambao wana dalili.
Je, ninawezaje kuzuia giardiasis?
Wewe na jamii yako mnaweza kuepusha giardiasis kwa:
Kuwa na maji ya umma yaliyosafishwa vizuri, ikijumuisha maji ya kunywa na maji yaliyo kwenye mabwawa ya kuogelea
Kunawa mikono kabla ya kuandaa chakula
Kunawa mikono vizuri baada ya kutumia choo
Kuepuka kugusana na kinyesi wakati wa kushiriki ngono
Kuchemsha maji yaliyochotwa kwenye mito na ziwa kabla ya kuyanywa