Maambukizi ya Minyoo

Imepitiwa/Imerekebishwa Jul 2023

Je, tegu ni nini?

Tegu ni minyoo mirefu yenye umbo la bapa, ambayo inafanana na kipande cha utepe au ribon. Kuna aina mbalimbali za tegu. Aina zingine zina urefu wa zaidi ya futi 15 (mita 4.5), na aina moja ina urefu wa zaidi ya futi 30 (mita 9).

  • Aina mbalimbali za tegu huishi katika minofu ya wanyama na samaki mbalimbali

  • Unapata tegu kwa kula chakula ambacho hakikuiva vizuri kinachotokana na wanyama wenye tegu katika nyama zao

  • Kisha tegu hukua ndani ya utumbo wako

  • Madaktari huchunguza kinyesi chako kutafuta tegu

  • Kwa kawaida vidonge vya minyoo huua tegu

  • Pika chakula chako vizuri ili usipate tegu

Je, nini husababisha maambukizi ya tegu?

Wanyama na samaki wakati mwingine hula vitu vilivyochafuliwa kwa mayai ya tegu. Mayai huanguliwa na kuingia kwenye misuli ya wanyama au samaki na kusababisha viuvimbe.

A Beef Tapeworm

Mara nyingi, unapata maambukizi ya tegu:

  • Unapokula nyama au samaki mwenye viuvimbe vya tegu ambaye hakupikwa vizuri

Viuvimbe hupasuka na kuingiza minyoo kwenye utumbo wako. Kisha tegu hujipachika kwenye utando wa utumbo wako na kukua.

Ni nadra sana, kwa watu kula vitu ambavyo vimechafuliwa kwa mayai ya tegu. Kisha tegu wanaweza kutengeneza viuvimbe kwenye misuli yako. Pia wanaweza kutengeneza viuvimbe kwenye ini, ubongo, na ogani zingine na kukufanya uumwe sana.

Je, ni wanyama wa aina gani wanaweza kunipa tegu?

Wanyama ambao huwa na tegu zaidi ambazo unaweza kupata ni:

  • Ng'ombe (tegu wa nyama ya ng'ombe)

  • Nguruwe (tegu wa nyama ya nguruwe)

  • Samaki wanaoishi kwenye maji baridi

Lakini wanyama wengine wengi hubeba tegu, ikiwa ni pamoja na mbwa, paka, kondoo na wanyama wengi wa mwituni.

Je, dalili za maambukizi ya tegu ni zipi?

Hata tegu wakubwa kwenye utumbo wako wanaweza wasisababishe dalili zozote. Unaweza kuhara kidogo au tumbo kuuma kidogo.

Viuvimbe vya tegu ambavyo hutokea kwenye mwili wako vinaweza kusababisha dalili kali kutegemea na sehemu vilipo:

  • Ubongo: Maumivu ya kichwa, kifafa, kuzimia, kifo

  • Uti wa mgongo: Udhaifu au kupooza

  • Ini: Maumivu ya tumbo, ngozi na macho ya njano (homa ya nyongo ya manjano)

  • Mapafu: Kikohozi, maumivu ya kifua

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina maambukizi ya tegu?

Madaktari hugundua tegu kwenye utumbo wako kwa:

  • Kutafuta mayai ya tegu kwenye kinyesi (choo kikubwa) chako kwa kutumia hadubini

Madaktari hugundua uwepo wa viuvimbe vya tegu kwenye ogani zako kwa vipimo vya upigaji picha kama vile uchanganuzi wa CT (tomografia ya kompyuta), au MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku).

Je, madaktari hutibu vipi maambukizi ya tegu?

Kwa kawaida dozi moja ya dawa za kuua tegu huua tegu waliopo kwenye utumbo wako.

Ikiwa una viuvimbe vya tegu kwenye ogani zako, unaweza kuhitaji kufanyiwa upasuaji ili kuviondoa.

Je, ninawezaje kuzuia maambukizi ya tegu?

Katika nchi nyingi, wakaguzi wa serikali hukagua nyama na samaki kama zina viuvimbe vya tegu. Hata hivyo, vitu muhimu vya kuzingatia ni:

  • Kupika vizuri nyama na samaki wa maji baridi

  • Kutokula samaki wabichi wa maji baridi

Kugandisha kunaweza kuua tegu wa samaki, lakini samaki anapaswa kugandishwa kwa siku 7 kwa halijoto ya -4° F (-20° C) au chini zaidi. Kubanika na kukausha nyama na samaki hakuui viuvimbe vya tegu.