Konjunktiva ni tishu iliyo wazi, nyembamba iliyo kando ya kope zako na hufunika weupe wa jicho lako.

Trakoma ni nini?

Trakoma ni aina fulani ya maambukizi ya bakteria ya konjunktiva.

  • Trakoma husababishwa na bakteria Chlamydia trachomatis

  • Ikiwa hautatibiwa, unaweza kupoteza uwezo wa kuona

  • Trakoma ni sababu inayoweza kuepukika zaidi ya upofu duniani

  • Trakoma mara nyingi huwapata watoto wadogo wanaoishi katika nchi kavu na zenye joto huko Kaskazini mwa Afrika, Mashariki ya Kati, India, Australia, na Asia ya Kusini-mashariki

  • Trakoma inasambaa kwa urahisi kwa kugusa jicho au mikono ya mtu aliyeambukizwa, na nzi, au kwa kushirikiana vitu vilivyo na maambukizi, kama vile taulo

  • Madaktari hutibu trakoma kwa kutumia dawa ya kuua bakteria

Je, nini husababisha trakoma?

Trakoma husababishwa na aina ya bakteria Chlamydia trachomatis Ugonjwa huo unasambaa kwa urahisi kwa:

  • Kugusa jicho lako baadaa ya kugusa jicho au mikono ya mtu aliyeambukizwa

  • Nzi

  • Kushirikiana taulo, vipodozi vya macho, au leso zilizo na bakteria

Bakteria hiyo inahusiana na aina ya klamidia ambayo husababisha maambukizi ya zinaa, lakini trakoma haisambazwi kingono.

Dalili za trakoma ni zipi?

Kwa kawaida macho yako yote mawili huathiriwa. Dalili za mapema zinajumuisha:

  • Macho mekundu yenye mwasho

  • Macho yenye majimaji

  • Kope zilizovimba

  • kuumizwa na mwanga mkali

Baada ya muda, trakoma huanza kuathiri konea yako polepole. Konea ni safu ya wazi mbele ya jicho lako ambayo kupitia hiyo unaweza kuona. Iko mbele, juu ya sehemu yenye rangi ya jicho lako (mboni). Wakati konea yako imeathiriwa na trakoma, una:

  • Matatizo ya kuona yanayozidi kuwa mabaya (kuona kunazuiwa na mishipa ya damu inayokua kwenye konea)

  • Makovu kwenye sehemu ya ndani ya ukope wako ambayo yanakwaruza konea yako na pia kusababisha kope zako kuelekea ndani na kusugua kwenye konea yako unapopepesa

  • Kupoteza uwezo wa kuona au upofu

Madaktari wanajuaje kama nina trakoma?

Madaktari hushuku trakoma kulingana na dalili zako. Ili kudhibitisha, watakusugua jicho lako na kutuma sampuli kwenye maabara.

Madaktari hutibu vipi trakoma?

Madaktari watafanya:

  • Kukupa dawa ya kuua bakteria (kupitia mdomo au kwa mafuta ya kuweka kwenye jicho lako)

  • Wanafanya upasuaji wa macho, ikiwa trakoma imesababisha madhara mabaya kwenye kope zako au imeharibu konea yako

Ninaweza kuzuiaje ugonjwa wa trakoma?

Ili kuzuia kueneza trakoma, madaktari watakuambia:

  • Unawe mikono na uoshe uso wako kwa maji safi

  • Usishiriki taulo, nguo za kuogea, na matandiko na watu wengine

  • Uondoe maeneo ambayo nzi wanaweza kuzaliana

Ikiwa watu wengi wanaoishi karibu na wewe wana trakoma, madaktari watampa kila mtu katika eneo lako dawa za kuua bakteria.