Polipu za Mapua

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2024

Je, polipu za pua ni nini?

Polipu za pua ni vinyama vinavyoota kwenye pua yako. Kwa kawaida huwa na umbo la yai na vinaweza kufanana kidogo na zabibu zilizomenywa.

  • Polipu za pua sio saratani

  • Una uwezekano mkubwa wa kupata polipu za pua ikiwa una mzio, pumu, au wanafamilia wenye polipu za pua

  • Polipu za pua zinaweza kuziba pua zako

  • Kwa kawaida madaktari hutibu polipu za pua kwa kutumia kotikosteroidi za kupuliza puani (ili kupunguza uvimbe), lakini wakati mwingine hufanya upasuaji

Je, nini husababisha polipu ya pua?

Madaktari hawajui ni kwanini hasa watu hupata polipu za pua. Hata hivyo, una uwezekano mkubwa wa kuzipata ikiwa una:

  • Maambukizi mengi ya sanasi

  • Pumu

  • Mizio, hasa mzio wa aspirini

  • Una wanafamilia wenye polipu za pua

Je, zipi ni dalili za polipu za pua?

Huenda usionyeshe dalili, lakini iwapo utakuwa nazo, zinaweza kujumuisha:

  • Pua kufungana

  • Pua zinazotoa kamasi

  • Kupiga chafya

  • Tatizo la kunusa

Je, madaktari wanawezaje kujua kama nina polipu za pua?

Madaktari, wanaweza kufahamu kuwa una polipu za pua kwa kutazama ndani ya pua yako.

Je, madaktari hutibu vipi polipu za pua?

Kwanza, madaktari hutibu polipu za pua kwa:

  • Kotikosteroidi za kupuliza puani

Ikiwa kinyunyizio hakitafanya kazi, madaktari wanaweza kukupatia vidonge vya kotikosteroidi

Ikiwa matibabu ya kotikosteroidi hayafanyi kazi, au polipu zimeziba pua kwa kiwango kikubwa, madaktari wanaweza kukufanyia upasuaji wa kuodnoa polipu.

Ili kuzuia polipu za pua zisirejee, madaktari wanaweza kukufanya uendelee kutumia kotikosteroidi za kupuliza puani.