Ugonjwa wa Kupooza kwa Ubongo

Imepitiwa/Imerekebishwa Apr 2024

Ugonjwa wa kupooza kwa ubongo (CP) ni nini?

CP ni hali ya ubongo inayoathiri misuli. Inafanya misuli kuwa ngumu na ugumu wa kusogea.

  • CP husababishwa na uharibifu wa ubongo unaotokea kabla, wakati, au muda mfupi baada ya kuzaliwa

  • Matatizo ya misuli yanaweza kuwa kiasi (migumu au goigoi) au makali (kutoweza kabisa kutembea au kusogeza misuli fulani)

  • Watoto wengi wenye CP wanaishi hadi kuwa watu wazima

  • Hakuna tiba.

  • Matibabu yanaweza kusaidia kupunguza dalili

Je, ni nini kinachosababisha CP?

CP husababishwa na uharibifu wa sehemu ya ubongo inayodhibiti misuli. Wakati mwingine sehemu nyingine za ubongo wa mtoto pia huharibika.

Watoto wengine huzaliwa na uharibifu wa ubongo. Uharibifu huu unaweza kusababishwa na:

  • Maambukizi kwa mama wakati wa ujauzito

  • Tatizo la jeni za mtoto

Ubongo wa baadhi ya watoto huharibika wakati wa kujifungua au mara tu baada ya kuzaliwa. Uharibifu wakati mwingine husababishwa na:

  • Ukosefu wa oksijeni wakati wa kujifungua

  • Maambukizi katika mtoto baada ya kuzaliwa

  • Ugonjwa mbaya wakati wa mwaka wa kwanza wa maisha ya mtoto

Watoto wachanga wanaozaliwa mapema (kabla ya wakati) na ambao wana uzito mdogo wana uwezekano mkubwa wa kuwa na uharibifu wa ubongo ambao unaweza kusababisha CP.

Je, dalili za CP ni zipi?

Watoto wanaweza kuwa na:

  • Mikono na miguu dhaifu na ngumu

  • Matatizo ya kutembea au kushindwa kutembea kabisa

  • Matatizo ya kunena

  • Macho yaliyopishana, mavivu, au yanayozunguka (huitwa makengeza) na matatizo mengine ya kuona

  • Matatizo ya kumeza

  • Mwendo usioweza kudhibitiwa, wa kutetemeka

Matatizo haya yanaweza kuwa ya kawaida hadi makali sana. Watoto walio na matatizo amdogo wanaweza kuonekana kuwa ni goigoi. Watoto walio na matatizo makubwa wanaweza kushindwa kutembea au hata kumeza chakula.

Watoto ambao wameharibika sehemu nyingine za ubongo wao wanaweza pia kuwa na matatizo ya kusikia, kujifunza, au tabia.

Je, madaktari watajuaje ikiwa mtoto wangu ana CP?

Madaktari wanaweza kufikiria mtoto wako ana CP ikiwa mtoto wako ni:

  • Amechelewa kujifunza kutembea

  • Amechelewa kukuza ujuzi mwingine

  • Ana umri chini ya miaka 2 na ana misuli migumu na dhaifu (huitwa kukakamaa kwa misuli)

Daktari kawaida hufanya MRI (upigaji picha kwa mvumo wa sumaku) ya ubongo wa mtoto wako ili kuangalia upungufu fulani katika ubongo. MRI ni uchanganuzi unaoonyesha picha za kina. Hata hivyo, hakuna kipimo kinachoeleza kwa uhakika ikiwa mtoto wako ana CP.

Je, madaktari wanatibuje CP?

Hakuna tiba ya CP. Hata hivyo, daktari wako na mtaalamu anaweza kupendekeza mambo mengi ili kumsaidia mtoto wako kutembea/kusogea vizuri, ikiwa ni pamoja na:

  • Viunga vya mkono au mguu ili kusaidia kudhibiti misuli na kutembea

  • Tiba ya kimwili ili kusaidia kuimarisha na kulegeza misuli

  • Tiba ya shughuli za kila siku ili kujifunza jinsi ya kufanya shughuli za kila siku, kama vile kupiga mswaki, kutumia uma, au kuchana nywele.

  • Tiba ya kuzungumza ili kusaidia kufanya matamshi yaeleweke na kujifunza jinsi ya kumeza kwa urahisi zaidi

  • Dawa za kusaidia misuli kulegea

Mtoto wako anaweza kunywa dawa kwa njia ya mdomo ili kusaidia misuli kulegea. Wakati mwingine, madaktari huingiza Botox kwenye misuli ya mtoto ili kuifanya kulegea. Ikiwa misuli ni migumu sana kiasi kwamba inazuia mtoto wako kusogeza mkono au mguu hata kidogo, madaktari wanaweza kufanya upasuaji. Katika upasuaji huo, madaktari hukata au kurefusha kano inayoshikanisha misuli migumu kwenye mfupa.