Una utumbo mdogo na utumbo mpana. Utumbo mdogo ni tyubu ndefu iliyojikunja ambayo huunganisha tumbo yako na utumbo mpana. Utumbo mkubwa (utumbo mpana) ni mfupi lakini pana na unaongoza kutoka mwisho wa utumbo mdogo hadi kwenye rektamu.
Ugonjwa wa Hirschsprung ni nini?
Utumbo mkubwa umejaa misuli ambayo hubana ili kusogeza kinyesi kupitia humo. Ugonjwa wa Hirschsprung ni kasoro ya kuzaliwa nayo ambapo sehemu ya utumbo mkubwa hukosa neva ambazo hutoa ishara kwa misuli ili kubana.
Kinyesi hujikusanya kwenye utumbo na kusababisha utumbo kuziba
Mtoto mwenye ugonjwa wa Hirschsprung anaweza kutapika, kukataa kula, na kuvimba tumbo
Madaktari hufanya upasuaji ili kuondoa sehemu ya utumbo ambayo haina neva
Iwapo hautatibiwa, ugonjwa wa Hirschsprung unaweza kusababisha maambukizi makali ya utumbo yanayoitwa enterokolaitisi
Dalili za ugonjwa wa Hirschsprung ni zipi?
Dalili zinajumuisha:
Kwa watoto waliozaliwa hivi karibuni, kutokujisadia ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa
Matapishi ya kijani au kahawia
Tumbo lililovimba
Kukataa kula
Ikiwa sehemu ndogo tu ya utumbo mpana wa mtoto imeziba, dalili zinaweza kuwa si kali na zinaweza kujumuisha:
Kinyesi chembamba, kama utepe
Tumbo lililovimba
Uzani kutoongezeka
Kutokutoa kinyesi
Watoto wenye dalili zisizo kali wanaweza kutotambulika kuwa na ugonjwa huo hadi baadaye utotoni au, kwa nadra, wakiwa tayari ni watu wazima.
Ikiwa ugonjwa wa Hirschsprung hautatibiwa, mtoto anaweza kupata Hirschsprung enterokolaitisi. Hii inaweza kwua ya kutishia maisha ikiambatana na dalili ambazo ni pamoja na:
Homa ya ghafla
Tumbo lililovimba
Mlipuko wa kuhara
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtoto wangu ana ugonjwa wa Hirschsprung?
Madaktari wanaweza kushuku uwepo wa ugonjwa wa Hirschsprung ikiwa mtoto wako hatatoa kinyesi ndani ya saa 24 tangu alipozaliwa.
Mdaktari hupima uwepo wa ugonjwa wa Hirschsprung kwa kutumia njia zifuatazo:
Eksirei ya bariumu kwa njia ya haja kubwa
Uondoaji wa kipande cha tishu kwenye rektamu kwa uchunguzi (madaktari hutoa kipande kidogo cha rektamu ya mtoto ili kukichunguza kwenye hadubini)
Kupima shinikizo ndani ya rektamu ya mtoto
Je, madaktari hutibu vipi ugonjwa wa Hirschsprung?
Madaktari hutibu ugonjwa wa Hirschsprung kwa:
Kufanya upasuaji wa kuondoa sehemu ya utumbo yenye kasoro na kuunganisha pande 2 za utumbo unaofanya kazi
Wakati mwingine, ikiwa mtoto anaumwa sana, kwanza madaktari hutoboa tundu la muda mfupi kwenye tumbo. Hutoboa tundu kwenye utumbo mpana na kuliunganisha na tundu la tumbo. Kinyesi cha mtoto wako hupitia kwenye tundu na kuingia kwenye mfuko hadi pale mtoto wako atakapokua na afya ya kutosha kuweza kufanyiwa upasuaji mwingine. Madaktari hufanya upasuaji ili kuondoa sehemu ya utumbo ambayo haifanyi kazi, kuunganisha tena utumbo unaofanya kazi, na kuziba tundu lilitobolewa tumboni.
Madaktari hutibu maambukizi (enterokolaitisi) kwa kutumia:
Kiowevu na dawa za kuua bakteria kupitia mishipa
Kuondoa kinyesi kwenye utumbo kwa kutumia maji ya chumvi yanayowekwa kupitia bomba kwenye rektamu
Upasuaji