Uzuiaji wa Saratani

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023 | Imebadilishwa Oct 2023

Ninawezaje kuzuia saratani?

Hakuna njia inayoweza kukuhakikishia kuwa kamwe hutapata saratani? Hata hivyo, baadhi ya mambo yanaweza kupunguza hatari ya kuugua aina fulani za saratani:

  • Usivute sigara na uepuke kuwa maeneo yenye moshi wa sigara: Saratani ya mapafu, figo, kibofu cha mkojo, kichwa, shingo, kinywa, na ulimi

  • Usitumie tumbaku isiyo na moshi (ya kunusa au kutafuna): Saratani ya kichwa, shingo, mdomo, na ulimi

  • Usinywe pombe kupita kiasi: Saratani ya kichwa, shingo, ini, na umio (tyubu inayounganisha koo yako na tumbo yako)

  • Usikae kwenye mwanga wa jua kwa vipindi virefu na utumie krimu ya kinga dhidi ya jua: Saratani ya ngozi

  • Kuwa mwangalifu kazini ili usigusane na kemikali zinazoweza kusababisha kansa: Kansa za aina mbalimbali

Pata chanjo zinazoweza kuzuia aina fulani za kansa zinazosababishwa na virusi:

Si kila mtu anahitaji chanjo hizo, kwa hivyo zungumza na daktari ili ujue iwapo unazihitaji.

Vipimo vya uchunguzi vya kubaini saratani mapema si mbinu za uzuiaji. Hata hivyo, matibabu ya saratani huwa na ufanisi zaidi yanapoanzishwa mapema. Zungumza na daktari wako ili ubaini iwapo unapaswa kupata vipimo vya uchunguzi kama vifuatavyo:

  • Mamogramu (eksirei ya matiti) ili kubaini saratani ya matiti: Wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 40 au 50

  • Kipimo cha virusi vya papiloma vya binadamu (HPV) na/au kipimo cha Pap ili kubaini saratani ya mlango wa kizazi: Wanawake wengi wenye umri wa kati ya miaka 21 na 65

  • Kolonoskopia au vipimo vingine vya kubaini saratani ya utumbo mpana: Watu wengi huanza katika umri wa miaka 45

Vipimo vingine vinaweza kufaa ikiwa uko katika hatari ya juu ya kuugua kansa za aina fulani (kwa mfano, kansa inayotokea sana kwenye familia yenu).

Ni hatua zipi zingine zinazoweza kusaidia kuzuia saratani?

Madakatari hawajui kwa uhakika iwapo lishe bora na mazoezi yanaweza kukuzuia usipate saratani, lakini huenda mambo hayo yakasaidia. Katika hali yoyote ile, ni vizuri ufanye mambo haya:

  • Kula vyakula visivyo na mafuta mengi, kama vile nyama na bidhaa za maziwa zenye kiwango kidogo cha mafuta

  • Punguza kiasi cha nyama zilizosindikwa unazokula, kama vile nyama za madukani

  • Kula matunda na mboga kwa wingi

  • Kula vyakula vingi vya nafaka kamili, kama vile mchele wa kahawia

  • Fanya mazoezi

  • Hakikisha uzani wako ni wa kiwango kinachofaa