Tiba ya Saratani ya Mfumo wa Kinga

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023

Ni nini maana ya tiba ya saratani ya mfumo wa kinga?

Tiba ya mfumo wa kingamwili ni aina ya matibabu ya saratani inayotumia mfumo wako wa kinga kupambana na saratani yako. Mfumo wako wa kingamwili una seli, tishu, na ogani za kukulinda dhidi ya magonjwa na maambukizi.

Mfumo wa kingamwili hufanya kazi kupitia mfulilizo wa vitendo viitwavyo hatua za kinga. Katika mfumo wa kinga:

  • Mwili wako hutambua kitu hatari ambacho hakipaswi kuwa mwilini mwako (antijeni)

  • Mwili wako huzalisha kingamwili na seli zinazoshambulia antijeni hiyo

Mfumo wako wa kingamwili mara nyingi hutambua kuwa seli za saratani ni hatari. Unapozitambua, unazishambulia na kuziharibu. Huwa hatugundui kansa nyingi ndogo ndogo ambazo huharibiwa haraka mara tu zinapoanza. Hata hivyo, kansa inapokuwa kubwa sana hivi kwamba inaonyesha dalili, kuna uwezekano kuwa mfumo wako wa kingamwili umeshindwa kuishambulia tena. Kwa sababu hiyo, madaktari wamebuni mbinu za kusaidia mfumo wako wa kingamwili kupambana na saratani.

Madaktari wanawezaje kutumia tiba ya mfumo wa kinga kukusaidia kupambana na saratani?

Kuna njia kadhaa tofauti ambazo madaktrai wanaweza kutumia kuimarisha utendaji wa mfumo wako wa kinga ili kusaidia mwili wako kupambana na saratani. Huenda daktari:

  • Kukupa aina za chembechembe za kingamwili zilizotengenezwa kwenye maabara za kulenga na kuharibu seli za saratani.

  • Kutoa seli (seli nyeupe za damu) kwenye mfumo wako mwenyewe wa kingamwili, kuzizidisha kwenye maabara, na kukupatia seli hizo tena

  • Kukupa dutu zinazoimarisha uwezo wa mfumo wako wa kingamwili wa kupata na kuua seli mahususi za saratani

  • Kukupa dawa zinazoweza kudhoofisha kinga ambazo seli za saratani zinatumia kujilinda dhidi ya mfumo wa kingamwili

Madaktari wanapotumia seli kutoka kwenye mfumo wako mwenyewe wa kingamwili, wakati mwingine wanatumia seli ambazo tayari zinajua jinsi ya kushambulia kansa, na wakati mwingine wanarekebisha seli hizo ili ziwe na ufanisi zaidi. Tiba nyingi za mfumo wa kinga hufaulu kwenye aina chache tu za saratani.