Je, lishe yako inaweza kusababisha au kuzuia saratani?
Madaktari wamefanya tafiti nyingi za kubaini iwapo lishe yako (kula vyakula vya aina fulani) kunaweza kuongeza au kupunguza uwezekano wako wa kupata saratani.
Madaktari hawajui kwa kweli iwapo baadhi ya vyakula na lishe vinaweza kuongeza au kupunguza uwezekano wako wa kupata saratani kwa sababu tafiti mbalimbali zimepata matokeo tofauti
Madaktari wanajua kwamba kuwa na uzani kupita kiasi au kuwa mnene kupita kiasi kutaongeza uwezekano wako wa kupata saratani
Baadhi ya aina za vyakula zimefanyiwa utafiti zaidi ya zingine, na madaktari wanazidi kutafiti athari za lishe katika kuugua saratani
Tafiti fulani zinaonyesha kuwa vitu vifuatavyo vinaweza kuongeza uwezekano wa kuugua saratani:
Vijalizo vya lishe vilivyo na kiwango cha juu cha vitamini A, vitamini E, au kalsiamu vinaweza kuongeza uwezekano wako wa kuugua saratani ya tezi dume
Vyakula vilivyo na kiwango cha juu cha mafuta yaliyokolea
Vyakula vilivyo na kiwango cha juu cha asidi ya mafuta ya omega-3, kama vile mafuta ya samaki vinaweza kuongeza uwezekano wako wa kuugua saratani ya tezi dume
Nyama zilizosindikwa, kama vile nyama za maandalizi ya haraka, nyama ya nguruwe, na soseji katika mkate, zinaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya tumbo na utumbo mpana
Nyama za kukaangwa au kuchomwa
Kiasi kikubwa cha chakula kilichohifadhiwa kwa achali au chumvi kinaweza kuongeza uwezekano wa kuugua saratani ya tumbo na koo
Viwango vya juu vya vijalizo vya lishe vya soya vinaweza kuongeza uwezekano wa kuugua saratani ya matiti
Tafiti fulani zinaonyesha kuwa yafuatayo yanaweza kupunguza uwezekano wa kuugua saratani:
Laikopini, inayopatikana sana kwenye nyanya
Viwango vya juu vya vitamini D na nyongeza ya kalsiamu inaweza kupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya utumbo mpana
Asidi ya foliki inaweza kupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya utumbo mpana
Vitamini D inaweza kupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya tezi dume na utumbo mpana
Yafuatayo yamefanyiwa utafiti na madaktari lakini hayajathibitishwa iwapo yanapunguza au kuongeza uwezekano wako wa kuugua saratani:
Vitamini au vitu vingine vilivyo na antioksidanti, kama vile seleniamu
Vyakula vilivyokuzwa kiasili, vilivyobadilishwa kijeni, au vilivyotibiwa kwa dawa za kuua vimelea
Kahawa na chai
Vyakula vilivyo na kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi
Floraidi kwenye maji au dawa ya meno
Viungio vilivyoongezwa kwenye vyakula
Kitunguu saumu
Vyakula vilivyotibiwa kwa mionzi ili kuua vidudu
Sakrani (unga wa kuongeza utamu)