Dawa Mbadala za Saratani

Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023

Ni vigumu kutibu saratani. Watu wengi bado hufa kutokana na saratani hata kama walipata matibabu bora zaidi ya kisasa. Kwa hivyo watu hutafuta mbinu mbadala zinazoweza kusaidia kutibu kansa. Wengi hujaribu dawa mbadala. Watu wanaweza kutumia dawa mbadala badala ya matibabu ya kawaida (yaliyozoeleka) au pamoja na matibabu hayo.

Dawa mbadala ni nini?

Dawa mbadala ni tofauti na dawa za kawaida kwa njia moja haswa. Dawa mbadala hazijafanyiwa majaribio ya kisayansi ili kuthibitisha iwapo zinafanya kazi au ni salama. Dawa zote zinazouzwa Marekani ni sharti ziwe zimeonyesha ithibati ya kutosha kuwa zinafanya kazi kabla ya madaktari kuruhusiwa kuzipendekeza kwa wagonjwa. Kwa hivyo, kwa kuwa hazijafanyiwa majaribio ipasavyo, dawa mbadala haziwezi kutangazwa kama dawa halisi. Dawa mbadala ni mitishamba au bidhaa za mitishamba ambazo zinaweza kuuzwa kama vijalizo vya lishe.

  • Aina nyingi za dawa mbadala hazijafanyiwa majaribio ya kisayansi ili zithibitishwe kuwa zinafanya kazi

  • Manufaa ya dawa mbadala hayajathibitishwa na zinaweza kukudhuru

Ni zipi hatari za kutumia dawa mbadala?

Huenda dawa mbadala:

  • Zisifaulu kutibu kansa yako

  • Zikazuia aina zingine za matibabu unazopokea, kama vile tibakemikali, zisifanye kazi

  • Zikagharimu pesa nyingi na hivyo kuifanya vigumu kwako kulipia matibabu ya kawaida kutoka kwa daktari wako

  • Baadhi zinaweza kusababisha athari za sumu

Mwambie daktari wako iwapo unatumia dawa mbadala za saratani ili kuzuia madhara.