Kufa kwa Ubongo

Imepitiwa/Imerekebishwa Dec 2022

Je, kufa kwa ubongo ni nini?

Kufa kwa ubongo ni pale ambapo ubongo wa mtu unapoacha kufanya kazi kabisa lakini mwili unabaki ukiwa hai kwa mashine za kupumua na dawa.

  • Watu ambao ubongo wao umekufa hawatambui chochote na hawafikiri wala kuhisi

  • Hawawezi kujisogeza wala kupumua

  • Ubongo wao huacha kudhibiti shughuli za mwili zisizo za hiari kama vile mapigo ya moyo na shinikizo la damu

  • Watu ambao ubongo wao umekufa kisheria, wanachukuliwa kuwa wameaga dunia

Mashine zinaweza kupumua kwa niaba ya mtu ambaye ubongo wake umekufa na dawa zinaweza kufanya moyo uendelee kudunda kwa muda mfupi. Hata hivyo, mwishowe, viungo vyote vya mtu huyo huacha kufanya kazi. Ikiwa mtu huyo alitaka kuchangia viungo, madaktari wanaweza kutumia viungo vya mtu huyo kwa upandikizaji. Lakini uchangiaji wa viungo unapaswa kufanyika kabla ya viungo kuacha kufanya kazi.

Hakuna mtu ambaye ubongo wake ulikufa aliyewahi kupona. Kufa kwa ubongo ni tofauti na kupoteza fahamu. Watu ambao wamepoteza fahamu ubongo wao una kiasi fulani cha utendakazi na wakati mwingine hupata afueni.

Je, nini husababisha kufa kwa ubongo?

Kufa kwa ubongo husababishwa na uharibifu mkubwa wa ubongo kuanzia:

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa ubongo wa mtu umekufa?

Kwanza madaktari huwa wanahakikisha kuwa mtu huyo hana tatizo lolote la kiafya ambalo linasababisha kupoteza fahamu kabisa sawa na kufa kwa ubongo. Matatizo hayo yanajumuisha:

  • Kuzidisha kiasi kinachohitajiwa cha dawa fulani

  • Joto la chini sana la mwili (hipothemia)

Ikiwa mtu hana mojawapo ya hayo matatizo, madaktari hufanya uchunguzi wa kimwili ili kubaini uwepo wa dalili za shughuli za ubongo ikiwa ni pamoja na:

  • Kujaribu kupumua ikiwa mashine ya kumsaidia kupumua itazimwa

  • Kushtuka au kusogea ikiwa mtu huyo atafinywa au kuchomwa kwa sindano

  • Kugooka kutokana na kitu kilichowekwa nyuma ya koo lake

  • Kupepesa jicho iwapo kitu kitagusa mboni ya jicho

  • Mboni kusinyaa kwa sababu ya mwanga wa tochi

Ikiwa hakuna dalili za shughuli za ubongo, wakati mwingine madaktari hurudia vipimo baada ya saa 6 hadi 24 ili kuhakikisha kwa mara nyingine tena kuwa mtu huyo haonyeshi kuitika. Baada ya kumpima mara mbili bila kuitikia, madaktari wanajua ya kwamba ubongo wa mtu huyo umekufa.

Badala ya kusubiri ipite siku moja ndipo warudie uchunguzi, madaktari wanaweza kufanya:

  • Vipimo vya mawimbi ya ubongo (EEG [elektroensefalografia]) ili kuona ikiwa ubongo una shughuli yoyote ya umeme

  • Vipimo vya mtiririko wa damu ili kuona kama kuna damu inayoingia kwenye ubongo

Watu ambao hawana shughuli za umeme au mtiririko wa damu kwenye ubongo wao huwa ubongo wao umekufa. Lakini vipimo hivi havihitajiki.

Je, madaktari hufanya nini iwapo mtu ana hali ya kufa kwa ubongo?

Kwa sababu kufa kwa ubongo kisheria humaanisha kuwa mtu amekufa, viungo vya mtu huyo vinaweza kutolewa kwa mtu ambaye ana uhitaji wa upandikizaji wa kiungo. Uchangiaji hauhitaji kusubiri hadi moyo wa mtu huyo uache kudunda. Viungo huchukuliwa ikiwa mtu huyo au familia yake inataka kuvitoa. Mashine ya kumsaidia kupumua au mashine za usaidizi huendelea kufanya kazi hadi jambo hili litimizwe. Viungo huondolewa kwa umakini, na mwili hushughulikiwa kwa heshima kubwa. Kisha madaktari:

  • Huzima mashine ya kumsaidia kupumua

  • Kusitisha dawa zozote

  • Kupeleka mwili kwenye ofisi ya afisa mchunguzi wa vifo au nyumba ya kuandaa mazishi