Je, uti wa mgongo ni nini?
Uti wa mgongo ni bomba refu lililoundwa kwa neva ambalo huanzia kwenye ubongo na kushuka chini hadi kwenye mgongo wako ukipita kwenye uwazi wa kati wa mgongo wako.
Uti wa mgongo ni kama kebo ya umeme ambayo husafirisha ujumbe kwenda na kurudi baina ya ubongo na mwili wako.
Kama mabavyo fuvu hulinda ubongo wako, mgongo hulinda uti wa mgongo wako, ambao ni rahisi kudhurika
Uti wa mgongo husafirisha ishara kutoka kwenye ubongo zinazouambia mwili wako cha kufanya, kama vile kusogeza mikono au miguu yako
Pia uti wa mgongo husafirisha ishara hadi kwenye ubongo kutoka kwenye mwili wako kama vile umegusa nini au sehemu gani yenye maumivu
Matendohisia (kama vile kuvuta mkono wako kutoka kwenye jiko la moto) hutokea kwenye uti wako wa mgongo pasipo ubongo wako kuhusika
Ikiwa uti wa mgongo wako umeharibika, kwa kawaida unapoteza uwezo wa kusogea au kuhisi sehemu za mwili wako
Je, uti wa mgongo hufanyaje kazi?
Seli za neva katika ubongo hutuma ujumbe hadi kwenye uti wa mgongo wako. Neva zingine kwenye uti wa mgongo wako hupokea ujumbe huu na kuutuma kwa mwili wako kupitia mojawapo ya neva za uti wa mgongo.
Seli za neva kwenye uti wa mgongo wako zina nyuzi za neva zilizosambaa kwenye mwili wako ambazo zimeunganishwa kwenye vipokezi vya hisia. Kwa mfano, kuna vipokezi vya hisia kwenye ngozi yako kwa ajli ya mguso na maumivu. Kitu chochote kinachochochea hivyo vipokezi vya hisia, kama vile kuchomwa na sindano, hutuma ishara kupitia nyuzi za neva hadi kwenye uti wa mgongo wako. Seli zingine za neva kwenye uti wa mgongo wako husafirisha ishara hiyo ya sehemu unapohisi maumivu hadi kwa ubongo wako.
Je, neva za uti wa mgongo ni nini?
Neva za uti wa mgongo ni neva za ukubwa wa wastani zinazounganisha uti wa mgongo na neva ndogo zinazoelekea sehemu mbalimbali za mwili wako. Zipo jozi 31 za neva za uti wa mgongo zinazoingia na kutoka kwenye uti wa mgongo kwenye nafasi kati ya vatabrae yako.
Kila neva ya uti wa mgongo huanzia sehemu maalum ya uti wa mgongo na kuelekea sehemu maalum kwenye mwili wako. Hivyo, kwa mfano, ukigusa sehemu mahususi kwenye ngozi yako, unahisi sehemu hiyo kwa sababu ya ujumbe uliotumwa kwenye ubongo wako kupitia neva mahususi ya uti wa mgongo.
Je, uti wa mgongo unaweza kupata matatizo gani?
Kuna matatizo mengi yanayoweza kuathiri uti wa mgongo wako, ikiwa ni pamoja na:
Majeraha
Saratani iliyoenea kwenye mgongo wako inaweza kuendelea hadi kwenye uti wa mgongo wako na kuuharibu
Kupoteza seli za neva za uti wa mgongo kutokana na magonjwa kama vile sklerosisi ya sehemu nyingi au kuzuiwa kwa usambazaji wa damu
Mara baada ya kufa kwa seli za neva katika uti wa mgongo, haziwezi kukua tena. Hivyo uharibifu wa uti wa mgongo kwa kawaida ni wa kudumu.
Ikiwa uti wa mgongo wako umeharibiwa, dalili zako hutegemea mahali ambapo uharibifu ulitokea. Kwa mfano, uti wa mgongo ukiharibika upande wa chini, huenda usiweze kusogeza au kuhisi chochote kwenye miguu yako lakini bado unaweza kutumia mikono yako. Lakini uti wa mgongo ukiharibiwa kwenye shingo, mikono na miguu yako yote huenda ikaathirika. Uti wa mgongo ukiharibika kwenye shingo yako, huenda usiweze kupumua. Huenda usiweze kudhibiti matumbo na kibofu cha mkojo, na huenda ukapoteza uwezo wa kushiriki ngono bila kujali sehemu ya uti wa mgongo wako uliyoharibiwa.