Viungo ni sehemu katika mwili wako ambapo mifupa miwili huungana, kama vile vifundo vya mikono, viwiko, mabega, nyonga, magoti na vifundo vya miguu.
Viungo pia vipo mahali ambapo hudhanii. Kwa mfano, kuna viungo kati ya mifupa mingi kwenye miguu, mikono, nyonga na uti wa mgongo.
Je, kukakamaa kwa viungo ni nini?
Kukakamaa viungo ni wakati kiungo hakiwezi kusogea kwa urahisi. Kukakamaa ni tofauti na kushindwa kusogeza viungo kwa sababu ya udhaifu au kutotaka kusogeza kiungo kwa sababu kina maumivu. Kukakamaa kwa viungo pia ni tofauti na misuli iliyokaza. Tatizo la misuli iliyokaza linaweza kutokana na kufanya mazoezi kupita kiasi au mara chache kutokana na matatizo kama vile polimyaljia reumatika au fibromyalgia.
Kukakamaa viungo kunaweza kusababishwa na majeraha au ugonjwa wa baridi yabisi
Kukakamaa kunaweza kuzidi asubuhi au kadiri muda wa siku unavyosonga
Kujinyoosha na tiba ya mazoezi inaweza kukusaidia kwenye tatizo ka kukakamaa
Ni nini husababisha kukakamaa kwa viungo?
Kwa kawaida kukakamaa kwa viungo husababishwa na:
Kushikilia kiungo bila kukisogeza kwa muda mrefu, kama vile wakati umefungwa plasta au banzi
Aina tofauti za ugonjwa wa baridi yabisi
Jeraha la kiungo lililopona (kama vile kutenguka)
Je, nitarajie nini ninapokwenda kumwona daktari wangu?
Daktari wako atakuuliza kuhusu dalili zako na kukufanyia uchunguzi wa kimwili.
Ikiwa madaktari hawana uhakika kama una ugonjwa wa baridi yabisi, wanaweza kufanya:
Vipimo vya damu
Eksirei
Madaktari wanatibu vipi tatizo la kukakamaa kwa viungo?
Madaktari watatibu kisababishaji cha kukakamaa huko.
Huenda pia madaktari wakalazimika kutibu hali yako ya kukakamaa kwa:
Kunyoosha
Kuwekelea kitu chenye joto kwenye kiungo, kama vile kwa kutumia pedi ya joto au manyunyu ya moto ya bafuni