Kile Ambacho Kila Mgonjwa Anapaswa Kujua Kuhusu Maambukizi ya Sinasitisi na Sinasi

Maoni25/02/25 Marvin P. Fried, MD, Montefiore Medical Center, The University Hospital of Albert Einstein College of Medicine

Baada ya siku kadhaa za kuumwa mafua, kile unachotaka tu ni kujisikia vizuri na kurejea katika hali ya kawaida. Lakini si kila mara jambo hilo hutokea.

Wakati mwingine kubanwa na mafua na pua kutoka kamasi kunaungana na uchovu na maumivu ya kichwa. Hizi zote ni ishara kwamba unaumwa maambukizi ya sinasi yanayojulikana kama sinasitisi. Sinasitisi ni moja ya magonjwa yaliyozoeleka sana, lakini hiyo haimaanishi, haitakusumbua utakapoipata. Njia bora ya kudhibiti dalili na kupunguza hatari za matatizo hatari zaidi ni kuelewa hali husika na hatua za kuitibu kwa ufanisi.

Haya ni mambo matano ambayo wagonjwa wanapaswa kuyajua kuhusu Sinasitisi ambayo yatawasaidia kuitofautisha na magonjwa ya mfumo wa hewa.

1. Sinasitisi inaweza kusababishwa na sababu nyingi

Kuna makundi mawili ya sinasi yanayozunguka mwanzi wa pua kwenye fuvu la kichwa. Sinasitisi ni neno la jumla kurejelea mwako wa sinasi zozote hizo. Mara nyingi, sinasitisi inasababishwa na maambukizi ya virusi kwenye sehemu ya juu ya mfumo wa upumuaji, kama vile mafua, kutengeneza mrundikano wa kiowevu. Hata hivyo, kuna sababu nyingine pia, ikiwa ni pamoja na mizio ya bakteria na ile ya msimu, inayoweza kusababisha kuvimba kunakosababisha sinasitisi, kama ilivyo kwa vitu kama vumbi au moshi. Baadhi ya kuvu zinaweza pia kusababisha maambukizi ya sinasi. Uvimbe utokanao na utando wa ute ute kwenye pua unaweza pia kuhusishwa na sinasitisi.

2. Kuna dalili za wazi za sinasitisi

Sinasitisi inahusiana kwa karibu na magonjwa mengine ya mfumo wa upumuaji na mara nyingi inaambatana na mwako wa kwenye mwanzi wa pua, ambao unasabisha kamasi kujaa na pua kutokwa na uchafu mzito au wenye rangi.

Lakini kuna dalili mahususi za kuangalia. Mara nyingi, sinasitisi huwa inakuwa na maumivu kuliko ugonjwa mwingine wa mfumo wa upumuaji. Mkazo kwenye sinasi unasababisha kuvimba na maumivu kwenye mashavu, maumivu nyuma ya macho au maumivu ya kichwa. Uchovu ni dalili nyingine muhimu. Watu wenye sinasitisi wanajihisi kuishiwa nguvu na kuchoka zaidi kuliko ambavyo wangekuwa na mzio au mafua.

3. Matibabu yanategemea ukali na muda

Muda ni kiashiria kingine muhimu cha sinasitisi. Mafua huwa yanadumu kati ya wiki moja hadi siku 10. Endapo hujisikii vizuri baada ya wiki mbili, ni muda wa kumwona daktari na kubaini kama una sinasitisi. Anza kwa kuweka miadi na daktari wako wa msingi na ujiandae kutoa maelezo ya kina kuhusu ugonjwa wako na dalili zake. Madaktari wanaweza kuitambua sinasitisi kulingana na maelezo hayo na uchunguzi wa kimwili. Katika mazingira fulani, wanaweza kuagiza uchanganuzi wa CT, ambao ni kiwango thabiti cha utambuzi wa ugonjwa.

Kwa visa vya sinasitisi kusababisha homa au maumivu makali na kudumu kwa zaidi ya siku 10, madaktari wanaweza kukuandikia dawa za kuua bakteria. Madaktari watapendekeza tiba za nyumbani ili kusaidia kukausha sinasi, ikiwa ni pamoja na

  • Kujifukiza
  • Taulo lililolowekwa kwenye maji ya moto na kufunika sinasi
  • Kunywa vimiminika vya moto
  • Kusukutua kwa maji ya chumvi
  • Kinyunyizio cha kupunguza msongamano wa kamasi puani

4. Sinasitisi inaweza kuwa sugu

Maambukizi mahususi ya sinasi pia yanajulikana kama sinasitisi kali. Sinasitisi inatafsiriwa kuwa ni sugu ikiwa imedumu kwa zaidi ya siku 90. Madaktari hawajui nini hasa husababisha sinasitisi sugu, lakini inajumuisha sababu ambazo zinasababisha mwako sugu. Sinasitisi inaweza pia kuwa kali kidogo (ikidumu kwa siku 30 hadi 90) au inayojirudia (vipindi 4 au zaidi vya sinasitisi kali kwa mwaka). Dalili za sinasitisi sugu zinafanana kwa ujumla na zile za sinasitisi kali.

Wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na sinasitisi sugu mara nyingi wanaelekezwa kwenda kwa daktari bingwa wa sikio, pua na koo (ENT). Matibabu huwa yanakuwa ya kina sana na yanaweza kujumuisha dawa za kuua bakteria zenye nguvu zaidi, steroidi za kumeza na matibabu mengineyo kwa awamu kadhaa. Hatimaye, upasuaji unaweza kupendekezwa kulingana na sababu ya sinasitisi.

5. Kutambuliwa kwa ugonjwa ni muhimu

Kuenea kwa maambukizi ya bakteria kwenye macho au ubongo kunaweza kusababisha hatari kubwa za kiafya. Ikiwa wewe au mpendwa wako anaumwa dalili za sinasitisi kwa zaidi ya siku 14, kutafuta huduma sahihi ni muhimu. Watoto, watu wazima na watu wenye kingamwili dhaifu wanapaswa kuwa makini zaidi.

Njia bora ya kuzuia sinasitisi na matatizo yake ni kuzuia maambukizi yasitokee kabisa. Hiyo ni rahisi kusema kuliko kutekeleza, hasa wakati wa msimu wa baridi. Lakini kufanya jitihada ili kudumisha afya kunaweza kuleta utofauti – nawa mikono yako na uache umbali unaofaa kati yako na watu wengine wanaoumwa. Na endapo utaugua, jitunze. Kupata usingizi wa kutosha na kuweka kipaumbele katika kupona vizuri ni njia nzuri za kuepuka sinasitisi.

Kwa maelezo zaidi kuhusu sinasitisi, tembelea ukurasa wa Mwongozo au Vidokezo vya Haraka kuhusu mada hii