Upasuaji wa kufungua mshipa

Moyo ni msuli unaopiga na kusukuma damu kwenye mwili wote. Ateri za moyo husambazia moyo wenyewe oksijeni na virutubishi muhimu inavyohitaji ili kufanya kazi inavyostahili.

Baada ya muda, mashapo ya mafuta yanayojulikana kama utando huenda yakajilimbikiza kwenye ateri, na kuziba njia na kuzuia mtiririko wa damu. Utando wa mafuta ukijilimbikiza kwenye ateri za moyo, mtiririko wa damu kwenye moyo unaweza kuathirika.

Upasuaji wa kufungua mshipa kwa kutumia puto ni upasuaji ambao hufungua ateri ambazo zimebanwa au kuzibwa kutokana na mrundiko wa utando wa mafuta. Wakati wa upasuaji huu, sindano hudungwa kwenye paja ili kufikia ateri ya nyonga. Kisha wavu huingizwa kwenye ateri ya nyonga na hupitishwa kwenye ateri hadi sehemu iliyozibwa.

Katheta ambayo imeunganishwa kwenye puto isiyo na hewa husogea pamoja na wavu hadi kwenye sehemu iliyozibwa. Puto inapotiwa hewa, inasukuma utando wa mafuta kwenye ukuta wa ateri hivyo kupanua ateri. Hatua hii huwezesha damu kuzunguka kama kawaida kupitia ateri.

Mara nyingi wakati wa upasuaji wa kufungua mshipa, kipanuzi cha mshipa huingizwa kwenye sehemu iliyozibwa ili kusaidia ateri kutojifunge tena. Kipanuz cha mshipa ni mrija wenye wavu unaowekwa karibu na katheta ya puto isiyo na hewa. Katheta inapoelekezwa kwenye eneo lililozibwa kisha kutiwa hewa, kipanuzi hupanuka na kugusa ukuta wa ateri. Kisha katheta na wavu zinaondolewa na mrija unasalia ndani.

Upasuaji wa kufungua mshipa na upasuaji wa kufungua mshipa kwa kutumia mrija huenda ukafanywa tena utando wa mafuta ukirundika tena.