Muhtasari wa Saratani wa Utotoni

NaKee Kiat Yeo, MD, Harvard Medical School
Imekaguliwa naMichael SD Agus, MD, Harvard Medical School
Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2024 | Imebadilishwa Jul 2024
v822501_sw

Nchini Marekani, matukio ya jumla ya saratani kwa watoto na vijana yameongezeka kadri muda unavyopita. Mnamo mwaka wa 2024, takribani visa 10,000 vya saratani vinatarajiwa kutambuliwa miongoni mwa watoto kuanzia kuzaliwa hadi umri wa miaka 14, na takribani visa 5,300 vya saratani vinatarajiwa kutambuliwa miongoni mwa vijana wa miaka 15 hadi 19. Hata hivyo, viwango vya vifo vimepungua kuanzia 1970 hadi 2020 kwa 70% kwa watoto na kwa 64% kwa vijana.

Licha ya maboresho katika viwango vya kuishi, saratani bado ni sababu kuu ya vifo miongoni mwa watoto. Nchini Marekani, saratani ndiyo sababu kuu ya pili ya vifo miongoni mwa watoto wa umri wa miaka 1 hadi 14 (ikizidiwa na ajali pekee) na ndiyo sababu ya nne kuu ya vifo miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 19.

Baadhi ya saratani za kawaida zinazotokea kwa watoto au vijana (kuanzia kuzaliwa hadi umri wa miaka 14) zinaweza pia kutokea kwa watu wazima:

Saratani zinazotokea kwa watoto pekee (kuanzia kuzaliwa hadi umri wa miaka 14) ni

Tofauti na saratani nyingi zinazowaathiri watu wazima, saratani zinazotokea hasa kwa watoto huwa na uwezo wa kutibika zaidi. Takribani 85% ya watoto na vijana walio na saratani huishi kwa angalau miaka 5. Nchini Marekani mwaka wa 2020, ilikadiriwa kuwa kulikuwa na watu wazima karibu 500,000 walionusurika saratani ya utotoni (yaani, ni watu wazima ambao walitambuliwa kuwa na saratani kwa mara ya kwanza kabla ya umri wa miaka 20).

Matatizo ya Matibabu ya Saratani

Kama ilivyo kwa huduma ya saratani kwa watu wazima, madaktari hutumia mchanganyiko wa matibabu, ikiwa ni pamoja na upasuaji, tibakemikali, uhamishaji wa chembe ya msingi, na tiba kwa njia ya eksirei, ili kutibu watoto wenye saratani. Tiba ya kinga mwili (aina mpya ya matibabu inayotumia mfumo wa kinga kushambulia saratani) na tiba inayolengwa (dawa zinazolenga mabadiliko mahususi ya jeni katika chembe za saratani na kuziharibu) zinachunguzwa na zinatumika mara nyingi zaidi kutibu saratani kwa watoto. Kwa sababu watoto bado wanakua, matibabu haya, hasa tibakemikali na tiba kwa njia ya eksirei, yanaweza kusababisha madhara ambayo kwa kawaida hayatokei kwa watu wazima. Kwa mfano, kwa watoto, mkono au mguu uliotibiwa kwa njia ya eksirei huenda usikue kabisa, au, ikiwa ubongo unatibiwa kwa njia ya eksirei, ukuaji wa ufahamu huenda usiwe wa kawaida. (Angalia pia Kanuni za Matibabu ya Saratani.)

Watoto wanaopona saratani wana miaka zaidi ya kupata matokeo ya muda mrefu ya tibakemikali, upasuaji, na tiba kwa njia ya eksirei, ambayo yanaweza kujumuisha

  • Utasa au Ugumba

  • Ukuaji duni

  • Kuchelewa au kutobalehe

  • Uharibifu kwa moyo na viungo vingine

  • Ukuaji wa saratani ya pili (ambayo hutokea kwa asilimia 3 hadi 12 ya watoto wanaopona saratani)

  • Matatizo ya kisaikolojia na kijamii

  • Matatizo ya ukuaji au neva au zote mbili

Kwa sababu matokeo mabaya kama hayo yanawezekana na matibabu ni changamano, watoto wenye saratani hutibiwa vyema katika vituo ambapo wataalamu wana uzoefu wa kutibu saratani za utotoni.

Hatari ya kupata saratani ya pili inategemea aina ya saratani ya kwanza. Hatari pia inategemea kama tiba kwa njia ya eksirei ilitumika kutibu saratani ya kwanza au ni aina gani ya tibakemikali ilitumika.

Timu ya utunzaji ya matibabu ya saratani

Athari za kutambuliwa kuwa na saratani na ukali wa matibabu zinaweza kumlemea mtoto na familia. Kudumisha hali ya kawaida kwa mtoto kunaweza kuwa vigumu, hasa kwa sababu mtoto anaweza kulazimika kulazwa hospitalini mara kwa mara na kutembelea ofisi ya daktari au kituo cha wagonjwa wasiolazwa kwa matibabu ya saratani. Ni kawaida kwa wazazi kuhisi mfadhaiko mkubwa wanapojitahidi kuendelea kufanya kazi, kuwazingatia ndugu, na bado kukidhi mahitaji mengi ya mtoto wao ambaye ana saratani (angalia Matatizo Sugu ya Afya kwa Watoto). Hali hii huwa ngumu hata zaidi mtoto anapopokea matibabu katika kituo maalum mbali na nyumbani.

Je, Ulijua...

  • Ingawa viwango vya visa vya saratani kwa watoto nchini Marekani vinaongezeka, viwango vya kupona pia vimeongezeka.

Watoto na wazazi wanahitaji timu ya matibabu ya watoto ili kusaidia kusimamia huduma. Madaktari wa watoto ni madaktari ambao ni wataalamu katika huduma na matibabu ya watoto wachanga, watoto na vijana. Timu hii kwa jumla inajumuisha wafuatao:

  • Wataalamu wa saratani ya watoto (daktari wa saratani ya watoto na daktari wa saratani wa tiba kwa njia ya eksirei)

  • Muuguzi wa saratani ya watoto, muuguzi aliyesajiliwa anayehudumia na kuwaelimisha watoto walio na saratani na familia zao

  • Wataalamu wengine wanaohitajika, kama vile daktari wa upasuaji wa watoto mwenye utaalamu wa kuondoa au kuchukua sampuli za kuchunguza saratani za utotoni, mtaalamu wa radiolojia wa watoto mwenye utaalamu wa kukagua tafiti za radiolojia (picha) kwa watoto wenye saratani, na mwanapatholojia mwenye utaalamu wa kutambua saratani za utotoni.

  • Daktari wa huduma ya msingi (daktari wa watoto)

  • Wataalamu wa maisha ya watoto, wanaoshirikiana na watoto na familia katika hospitali na mazingira mengine ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kulazwa hospitalini, magonjwa na ulemavu.

  • Mfanyakazi wa huduma za jamii, anayeweza kutoa msaada wa kihisia na kusaidia katika masuala ya kifedha ya huduma

  • Mwalimu, anayeweza kushirikiana na mtoto, shule, na timu ya matibabu ili kuhakikisha kwamba elimu ya mtoto inaendelea

  • Afisa wa ushirikiano na shule, ambaye pia anaweza kumsaidia mtoto na familia kuwasiliana na mwalimu na shule

  • Mwanasaikolojia, anayeweza kumsaidia mtoto, ndugu na wazazi kuhusu afya yao ya akili wakati wote wa matibabu

Timu nyingi za matibabu pia zinajumuisha mtetezi wa mzazi. Mtetezi wa mzazi ni mzazi mwingine aliyekuwa na mtoto mwenye saratani na anayeweza kutoa mwongozo kwa familia.

Watoto ambao wametambuliwa hivi majuzi kuwa na saratani wanapaswa kutathminiwa na timu ya kijenetiki ya saratani kwa mabadiliko ya kijenetiki yanayoweza kusababisha watu kupata saratani au yanaweza kuwa na athari kwenye matibabu.

Taarifa Zaidi

Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa MWONGOZO hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.

  1. The American Cancer Society: Ikiwa Mtoto Wako Ametambuliwa kuwa na Saratani: Rasilimali kwa wazazi na wapendwa wa mtoto ambaye ana saratani ambayo hutoa taarifa kuhusu jinsi ya kukabiliana na baadhi ya matatizo na maswali yanayojitokeza mara tu baada ya mtoto kugunduliwa na ugonjwa huo

  2. The American Cancer Society: Ukweli na Takwimu za Saratani 2024: Nyenzo inayotoa maelezo kuhusu aina mahususi za saratani, ikiwa ni pamoja na idadi ya visa vipya vya saratani na vifo, takwimu za kupona na taarifa kuhusu dalili