Je, C. diff ni nini?
Koloni yako ni utumbo wako mpana. Kolaitisi ni kuvimba kwa utumbo mpana. Klostridioidesi difisile ni bakteria inayosababisha kolaitisi. Ukiwa na kolaitisi, utakuwa unahara (kinyesi chepesi chenye majimaji) na dalili zingine. Klostridioide difficile na ugonjwa ambao inasababisha mara nyingi huitwa C. difficile au C. diff.
Dalili zinatofautiana kutoka kwa kuharisha kidogo hadi kuharisha damu mara kwa mara pamoja na maumivu ya tumbo na homa
Ili kujua kama una C. diff, madaktari hupima kinyesi (haja kubwa) na wakati mwingine hutumia mrija wa kuangalia ili kuangalia utumbo wako mpana
Una uwezekano mkubwa wa kupata C. diff baada ya kutumia dawa za kuua bakteria kwa ajili ya kutibu ugonjwa tofauti
Watu walio na C. diff wakati mwingine hupata nafuu wanapoacha kutumia dawa ya kuua bakteria ambayo ilisababisha tatizo
Ikiwa hali ya kuharisha haikomi au ni mbaya zaidi, unahitaji kutumia dawa nyingine ya kuua bakteria ili kuua bakteria aina ya C. diff
Je, ni nini husababisha C. diff?
Aina nyingi za vijidudu (viumbe vidogo) kwa kawaida huishi ndani ya utumbo wako mpana. C. diff ni mojawapo ya vijidudu hivyo. Kwa kawaida vijidudu hivi havina madhara. Hata hivyo, wakati mwingine, mojawapo ya vijidudu hivyo hukua na kuwa nje ya udhibiti na kukufanya kuwa mgonjwa. C. diff inapokua na kuwa nje yaudhibiti, hutengeneza dutu (sumu) ambayo huumiza utando wa utumbo wako na kusababisha kuhara.
Kumeza dawa za kuua bakteria kwa maambukizi tofauti ndiyo chanzo kikuu cha C. diff kukua na kusababisha maambukizi. Dawa za kuua bakteria huvuruga uwiano wa bakteria tofauti kwenye utumbo wako na kuruhusu C. diff kuchukua nafasi yake.
Hatari ya kupata C. diff. huongezeka kadri unavyozeeka. Hatari hiyo pia ni kubwa miongoni mwa watoto wachanga na watoto wadogo. Sababu zingine za hatari ni:
Kuwa na ugonjwa sugu
Kulazwa kwa muda mrefu hospitalini
Kuishi katika makazi ya huduma za uuguzi
Kufanya upasuaji kwenye tumbo au matumbo
Wakati mwingine, madaktari hawajui ni kwa nini mtu anapata C. diff.
Je, dalili za C. diff ni zipi?
Mara nyingi dalili huanza siku 5 hadi 10 baada ya kuanza kutumia dawa za kuua bakteria kwa maambukizi mengine. Lakini huenda usiwe na dalili hadi miezi 2 baada ya kuacha kutumia dawa za kuua bakteria.
Dalili huanzia kuhara kidogo hadi:
Kuhara damu
Maumivu ya tumbo
Homa
Kwa nadra, kuhisi kichefuchefu au kutapika
Hali mbaya zaidi inaweza kusababisha matatizo makubwa, kama vile:
Upungufu wa maji mwilini (maji kidogo sana mwilini mwako)
Shinikizo la chini la damu
Kuvimba kwa njia ya utumbo mpana kunakosababisha hatari
Tundu kwenye utumbo wako mpana
Je, madaktari wanawezaje kujua kuwa nina C. diff?
Madaktari hushuku C. diff ikiwa unahara ndani ya:
Miezi 2 baada ya kutumia dawa ya kuua bakteria
Saa 72 za kulazwa hospitalini
Kisha madaktari hutafuta:
C. diff na sumu yake katika sampuli ya kinyesi
Kuvimba (kolaitisi) na mabadiliko mengine katika utumbo wako mpana kwa kuangalia ndani yake kwa mrija wa kuangalia
Je, madaktari hutibu vipi C. diff?
Madaktari hutibu C. diff kwa:
Kusitisha matumizi ya dawa ya kuua bakteria iliyosababisha tatizo
Kutoa dawa ya kuua bakteria ya kumeza ambayo inakandamiza C. diff
Hupaswi kumeza dawa ambazo hupunguza kasi au kusimamisha kuhara. Hiyo huweka sumu ya C. diff kwenye utumbo wako na inaweza kukufanya kuhisi mgonjwa zaidi.
Mtu mmoja kati ya 5 ana dalili zinazorejea, wakati mwingine tena na tena. Ili kusaidia kuzuia dalili kurejea, huenda ukapata:
Dawa za kuua bakteria za muda mrefu
Probiotiki (tembe zinazoweza kusaidia kurejesha uwiano wa bakteria kwenye utumbo wako)
Upandikizaji wa kinyesi (kinyesi chenye afya cha mtu huwekwa kwenye utumbo wako ili kusawazisha bakteria)
Ikiwa dalili ni mbaya sana, unaweza kuhitajika kulazwa hospitalini ambapo madaktari watakupa:
Dawa za kuua bakteria
Majimaji kwenye mshipa wako
kuongezewa damu
Kwa nadra, madaktari hufanya upasuaji ili kuondoa utumbo ulioambukizwa sana.