Ambliopia

(Macho Matepetevu)

Imepitiwa/Imerekebishwa Sept 2023

Je, ambliopia ni nini?

Ambliopia (pia huitwa macho matepetevu) ni aina fulani ya upotevu wa uwezo wa kuona kwa watoto. Ikiwa picha zilizotumwa kwenye ubongo kutoka kwenye kila jicho hazifanani, basi ubongo hupuuza kile kinachoonwa na jicho moja.

  • Mara nyingi ambliopia huanza kabla ya umri wa miaka 2, lakini inaweza kuwapata watoto wa hadi umri wa miaka 8

  • Ambliopia inaweza kusababishwa na tatizo la kufokasi, macho ambayo hayawezi kujipanga baina yake, au mtoto wa jicho (ukungu kwenye lenzi ya jicho)

  • Watoto wanaweza kupoteza uwezo wa kuona moja kwa moja ikiwa ambliopia haijatibiwa kufikia umri wa miaka 8

  • Madaktari hurekebisha ambliopia kwa kutumia miwani ya macho, kitambaa cha kufunga kwenye jicho, au dawa ya matone ya macho

Je, nini husababisha ambliopia?

Uwezo wa watoto kuona huwa haujakomaa kikamilifu wakati wanapozaliwa. Watoto wachanga na watoto wadogo wanahitaji kuona picha safi, zilizolengwa kutoka kwa kila jicho ili njia zao za kuona zikue kama kawaida. Njia za kuona hazimalizi kukua hadi watoto wanapofikisha kiasi cha umri wa miaka 8.

Ikiwa ubongo wa mtoto haupokei picha nzuri za kuona kutoka kwa jicho moja, ubongo utaanza kulipuuzia jicho hilo. Kwa kipindi kifupi hili halina shida. Kama ambavyo ungefunga kitambaa kwenye jicho, bado ungeendelea kuona vizuri pale utakapokuondoa. Lakini ikiwa ubongo wa mtoto haupokei picha nzuri kutoka kwenye jicho moja, basi akifikisha umri wa kiasi cha miaka 8, ubongo wa mtoto hauwezi tena kujifunza kuona vitu kutoka kwenye hilo jicho hata kama tatizo la awali litarekebishwa. Jambo hili linaweza kusababisha tatizo la kudumu la upungufu wa uwezo wa kuona.

Ubongo unaweza ukaanza kupuuzia picha kutoka kwenye jicho moja kwa sababu:

  • Jicho hilo haliwezi kufokasi vizuri

  • Jicho hilo halitazami katika uelekeo ambao ni sawa na jicho jingine (tatizo linalojulikana kama makengeza)

  • Kuna kitu kimeweka ukungu au kinazuia uwezo wa jicho kuona, kama vile mtoto wa jicho au jicho lililoshuka chini

Dalili za ambliopia ni zipi?

Watoto wenye ambliopia hawawezi kuona vizuri kwa jicho moja. Huenda wasitambue kuwa wana tatizo au wanaweza kuwa wachanga sana kuelezea tatizo lao la kuona. Hata hivyo, watoto wenye ambliopia wanaweza:

  • Kuwa na makengeza au kufunika jicho moja

  • Kuwa na jicho moja ambalo halitazami katika uelekeo ambao ni sawa na ule wa jicho jingine

  • Kuwa na shida ya kutambua umbali uliopo baina ya vitu 2 (udhaifu wa kutambua kina), kwa mfano, kupata shida ya kudaka mpira

Madaktari wanawezaje kujua kama mtoto wangu ana ambliopia?

Ili kujua kama mtoto wako ana ambliopia au matatizo mengine ya kuona, madaktari hupima macho ya mtoto wako mara kwa mara. Kwa kawaida hufanya vipimo hivi katika ziara za kawaida za mtoto wako, kuanzia anapokuwa na umri wa miaka 3. Uwezo wa kuona wa mtoto wako unapaswa kuchunguzwa katika kipindi chote cha utoto wake.

Ikiwa madaktari watahisi kuwa mtoto wako haoni vizuri, watakufanya umpelke mtoto wako kwa daktari wa macho (mtaalamu wa macho au mpimaji wa macho).

Je, madaktari wanatibu vipi ambliopia?

Ili kutibu ambliopia, madaktari wa macho lazima waufundishe ubongo wa mtoto wako kutumia picha za kuona zinazotoka kwenye jicho lenye tatizo. Huenda daktari akafanya yafuatayo:

  • Huzuia kuona kwa jicho la mtoto wako ambalo halina shida kwa kuliziba na kitambaa au kwa kutumia matone kufifisha uwezo wake wa kuona—jambo hili hulazimisha ubongo kutambua picha zinazotoka kwenye jicho lenye tatizo

Ikiwa mtoto wako ana tatizo la kufokasi kama tatizo la kuona vizuri vitu vilivyo mbali kuliko vilivyo karibu, madaktari:

  • Watampatia miwani ya macho mtoto wako (au lenzi za kubandika kwenye macho)

Ikiwa mtoto wako ana makengeza au mtoto wa jicho, kwa kawaida madaktari:

  • Watafanya upasuaji wa jicho