Je, thrombosaitopenia ya kingamwili (ITP) ni nini?
Thrombosaitopenia ni chembe sahani, ambazo ni seli ndogo zinazozunguka kwenye mtiririko wa damu na kusaidia damu kuganda. Thrombosaitopenia ni hali ya kuwa na idadi ndogo sana ya chembe sahani kwenye damu yako.
Thrombosaitopenia ya kingamwili ni wakati unapokuwa na idadi ndogo sana ya chembe sahani kwa sababu mfumo wa kingamwili wako unaziharibu.
Kwa kuwa na idadi ndogo sana ya chembe sahani, unavuja damu kwa urahisi
Huenda ukapata madoa madogo ya zambarau kwenye ngozi yako na kutokwa damu puani na kwenye fizi
Madaktari hutambua uwepo wa ITP kupitia vipimo vya damu
Katika watoto, kwa kawaida ITP huondoka yenyewe
Watu wazima wenye ITP wanaweza kutumia kotikosteroidi au dawa zinginge ili kupunguza uwezo wa mfumo wa kingamwili
Iwapo wewe ni mtu mzima na dawa zimeshindwa kufanya kazi, madaktari wanaweza kuondoa bandama yako
Je, nini husababisha ITP?
ITP hutokea pale mfumo wako wa kingamwili unapotengeneza kingamwili ambazo hushambulia na kuharibu chembe sahani. Madaktari hawajui kwanini hali hii hutokea, lakini katika watoto mara nyingi hutokea baada maambukizi ya kirusi.
Je, dalili za ITP ni zipi?
Dalili za ITP zinaweza kutokea kwa ghafla au taratibu. Unaweza kuwa na:
Madoa madogo mekundu kwenye ngozi au mdomoni mwako
Michubuko baada ya majeraha madogo sana
Fizi kuvuja damu
Hedhi nzito
Uwezekano ni kuwa, chembe sahani ikipungua, utavuja damu zaidi. Walio na vigandisha damu vichache huenda wakavuja damu nyingi kwenye matumbo yao au maisha yao yakawa hatarini kwa kuvuja damu kwenye ubongo.
DKT P. MARAZZI/MAKTABA YA PICHA ZA KISAYANSI
DKT P. MARAZZI/MAKTABA YA PICHA ZA KISAYANSI
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina ITP?
Madaktari hufanya:
Vipimo vya damu vya kuhesabu idadi ya chembe sahani katika sampuli ya damu
Vipimo vya kutafuta sababu zingine zinazosababisha idadi ndogo ya chembe sahani
Mara chache, madaktari huchukua sampuli ndogo ya uboho wa mifupa (uondoaji wa sehemu ya uboho kwa ajili ya uchunguzi) ili kuchunguza ubora wa mwili wako katika kuzalisha chembe sahani.
Je, madaktari hutibu vipi ITP?
Madaktari hutibu ITP kwa:
Kotikosteroidi
Dawa ya kusaidia mwili wako kutengeneza chembe sahani nyingi zaidi
Dawa za kupunguza kasi ya mfumo wako wa kingamwili
Mara chache, upasuaji wa kuondoa bandama (splenektomi)
Ikiwa una uvujaji wa damu wenye kutishia maisha, madaktari wanaweza kukufanyia upandikazaji wa chembe sahani. Kwa kawaida upandikizaji wa chembe sahani haufanyi kazi vizuri kwa sababu kingamwili zilizopo kwenye damu yako hushambulia chembe sahani zilizopandikizwa.
Kuondoa bandama kunaweza kusaidia kudumisha chembe sahani nyingi zaidi zinazozunguka kwenye damu.
Kwa watu wazima, kwa kawaida ITP hudumu kwa kipindi kirefu, lakini kwa watoto hali huimarika yenyewe.