Rosacea

(Rosasia ya Chunusi)

Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2023

Rosasia ni nini?

Rosasia ni ugonjwa wa ngozi ambao hufanya pua yako na eneo linaloizunguka kuwa jekundu, kuvimba, na kufunikwa na chunusi ndogo na mishipa ya damu iliyovimba.

  • Rosasia huwapata zaidi watu wenye umri wa miaka 30 hadi 50, hasa watu wenye asili ya Ireland na Ulaya ya Kaskazini

  • Wakati mwingine rosasia hufanana chunusi

  • Matibabu yanajumuisha dawa za kuua bakteria

  • Kuepuka baadhi ya vyakula, pombe, vinywaji vya moto, mwanga wa jua, joto kali, upepo, na vipodozi kunaweza kukusaidia kupunguza dalili

Je, nini husababisha rosasia?

Madaktari hawajui kinachosababisha rosasia. Walio na ngozi nyororo wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huu.

Ikiwa tayari una rosasia, dalili zako zinaweza kuchochewa na:

  • Vyakula vyenye viungo vingi

  • Pombe

  • Vinywaji vya moto

  • Malai ya kuzuia miale ya jua au vipodozi

  • Msongo wa mawazo

  • Hali ya hewa ya baridi au joto, mwanga wa jua, au upepo

  • Mazoezi au kuoga maji ya moto

  • Dawa fulani

Dalili za rosasia ni zipi?

Rosasia hukuathiri uso na kichwani pekee. Kwa kawaida hali yake huzidi kuwa mbaya baada ya muda (miaka au miongo).

  • Kwanza, ngozi ya mashavu yako na pua huwa nyekundu kwa kipindi kirefu kuliko kawaida na inaweza kuchoma lakini vinginevyo ni kawaida

  • Ikiwa rosasia itaendelea, mara nyingi ngozi yako huwa na mwonekano mwekundu na kuvimba, yenye mishipa midogo ya damu yenye kuonekana chini tu ya tabaka la juu la ngozi

  • Unaweza kupata vichunusi vidogo

  • Katika hatua za mwisho, ngozi ya pua yako huongezeka unene, hivyo kuonekana nyekundu na iliyovimba

Pia rosasia inaweza kuathiri macho yako. Dalili zinajumuisha:

  • Kuvimba kwa vigubiko vya macho au macho

  • Kuwasha

  • Wekundu

  • Hisia kama kuna kitu kwenye jicho lako

Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina rosasia?

Daktari anaweza kubaini ikiwa una rosasia kwa kuangalia uso na kichwa chako.

Je, madaktari hutibu vipi rosasia?

Madaktari hutibu rosasia kwa njia zifuatazo:

  • Malai ya dawa za kuua bakteria au vidonge amabvyo vinafanana na vile vinavyotumika kwa chunusi

  • Jeli ya brimonidine au malai ya oksimetazolini kupunguza wekundu

  • Kwa mishipa ya damu inayoonekana, leza au elektrokodari (mkondo wa umeme kwenye ngozi yako ili kutibu mishipa ya damu inayoonekana)

  • Kwa pua yenye ngozi nene, kusugua ngozi (hatua ya kusugua na kuondoa ngozi ya ziada); au upasuaji ili kuondoa ngozi ya ziada

Pia madaktari watakufanya ujiepushe na vitu vinavyochochea rosasia yako.