Ugonjwa wa hisia mseto ni nini?
Ugonjwa wa hisia mseto ni tatizo la akili ambalo lina vipindi vya mfadhaiko na vipindi vya uchangamfu.
Mfadhaiko ni kuhisi huzuni nyingi hivi kwamba huwezi kufanya shughuli za kila siku au hivi kamba hutaki kufanya vitu ambavyo ulifurahia kuvifanya hapo awali.
Uchangamfu ni hali ambapo una hamasa na kujiamini kwa kiwango kikubwa, mawazo yako yanavurugwa kwa urahisi, na unafanya maamuzi hatarishi.
Ugonjwa wa hisia mseto kwa kawaida huanza ukiwa kijana au katika miaka ya 20 au 30
Kuna uwezekano kuwa ugonjwa wa hisia mseto ni wa kurithishwa katika familia
Hali yako mara nyingi itakuwa ya kawaida wakati hauna kipindi cha mfadhaiko au uchangamfu
Madaktari hutibu ugonjwa wa hisia mseto kwa kutumia dawa na matibabu ya kisaikolojia
Kuna aina 2 za ugonjwa wa hisia mseto, hisia mseto 1 na hisia mseto 2.
Ikiwa una ugonjwa wa hisia mseto 1, unapata:
Angalau kipindi 1 cha uchangamfu kinachokuzuia kufanya shughuli za kila siku na kinaweza kujumuisha maono ya uwongo (wakati ambapo unashindwa kujua vitu vya kweli)
Kwa kawaida vipindi vya mfadhaiko
Ikiwa una ugonjwa wa hisia mseto 2, unapata:
Angalau kipindi 1 cha uchangamfu usiokithiri (uchangamfu mdogo)
Vipindi vya mfadhaiko mbaya
Je, ni nini husababisha ugonjwa wa hisia mseto?
Madaktari hawajui haswa kinachosababisha ugonjwa wa hisia mseto. Jeni zako (maelezo ya kijenetiki unayopata kutoka kwa wazazi na mababu zako) zinaweza kuchangia.
Nyakati za uchangamfu (vipindi vya kuchangamka) zinaweza kuchochewa na
Kuongezeka au kupungua kwa kemikali fulani (visafirishaji ujumbe au ishara vya neva) katika mwili wa mtu—visafirishaji ujumbe au ishara vya neva ni kemikali kama vile serotonin na norepinephrine ambazo seli za neva hutumia kutuma ujumbe kwenye ubongo na mwili
Uvimbe wa ubongo au matatizo mengine ya ubongo
Tukio la mfadhaiko
Dawa za kulevya, kama vile kokeni
Matatizo mengine ya kiafya, kama vile matatizo ya tezi dudumio
Ni zipi dalili za ugonjwa wa hisia mseto?
Nyakati (vipindi) za mfadhaiko au uchangamfu huja na kutoweka. Hapo katikati, hali yako inaweza kuwa ya kawaida. Vipindi vya mfadhaiko na uchangamfu vinaweza kudumu kwa wiki kadhaa au hadi miezi 6.
Dalili za mfadhaiko:
Kuhisi huzuni sana
Kupungua kwa hamu ya kushiriki katika shughuli, hata zile ulizokuwa ukizipenda zamani
Kufikiria na kutembea polepole
Kuhisi majisuto na kukosa matumaini
Kulala kwa muda mrefu kuliko kawaida
Kuona vitu ambavyo si vya kweli
Dalili za uchangamfu:
Hisia ya kujiamini sana na kufikiria kuwa unaishi maisha mazuri
Kuwa na hamasa kubwa
Kuudhika haraka
Kulala kwa muda mfupi kuliko kawaida
Kuongea zaidi
Kuvurugwa mawazo kwa urahisi na kubadilisha kutoka kwa shughuli moja hadi nyingine
Kushiriki katika shughuli hatarishi, kama vile kamari au ngono, bila kufikiria kuhusu athari zake
Wakati mwingine kuona na kusikia vitu ambavyo si vya kweli
Watu walio na vipindi vya uchangamfu uliokithiri (ukichaa kupita kiasi) wanaweza kuwa na dalili kama vile:
Imani potofu kuwa wao ni watu wa kipekee, kama vile kuwa wao ni yesu au wana kipaji maalum
Kufikiria kuwa watu wanawafuata
Shughuli kupita kiasi, kama vile kukimbia huku na kule, kupiga mayowe, na kuimba
Kutotenda au kutofikiria kwa busara
Watu walio na uchangamfu kupita kiasi wanahitaji kwenda hospitalini mara moja.
Madaktari wanawezaje kujua iwapo nina ugonjwa wa hisia mseto?
Madaktari wanashuku kuwa una ugonjwa wa hisia mseto kulingana na mtindo wa dalili zako. Ukiwa na tatizo la uchangamfu kupita kiasi, huenda usiweze kuripoti dalili zako kwa usahihi kwa sababu hufikiri kuwa una tatizo lolote. Kwa hivyo madaktari wanaweza kuomba maelezo kutoka kwa wanafamilia.
Madaktari wanaweza pia kufanya vipimo vya damu au mkojo ili kuangalia iwapo dawa au matatizo mengine ya kiafya yanasababisha dalili zako.
Madaktari hutibu vipi ugonjwa wa hisia mseto?
Huenda daktari:
Kupendekeza dawa, kama vile lithium au valproate
Kutoa usaidizi wa ushauri nasaha wa kibinafsi au vikundi (matibabu ya kisaikolojia)
Dawa zisiposaidia tatizo lako la mfadhaiko, watakupatia tiba ya mshtuko wa umeme (ambayo awali iliitwa tiba ya kushtua ubongo)
Katika tiba ya mshtuko wa umeme, daktari wako atakupa dawa ili ulale kisha atapitisha umeme kwenye ubongo wako. Madaktari hawajui kwa nini, lakini umeme mara nyingi husaidia kuondoka mfadhaiko.
Ikiwa una tatizo la uchangamfu au mfadhaiko kupita kiasi na unafanya vitendo hatarishi vinavyoweza kusababisha matatizo mabaya, madaktari wanaweza kukutibu hospitalini