Skoliosisi ni nini?
Skoliosisi ni upinde usio wa kawaida kwenye uti wa mgongo
Watoto wanaweza kuzaliwa wakiwa na skoliosisi, au inaweza kuwapata watoto wa umri wa miaka 10 hadi 16.
Skoliosisi inaweza kufanya mabega na nyonga za mtoto wako zisilingane
Skoliosisi husababishwa na nini?
Kwa kawaida, sababu haiwezi kugunduliwa. Wakati mwingine, skoliosisi husababishwa na kasoro ya kuzaliwa.
Dalili za skoliosisi ni zipi?
Skoliosisi isio kali huwa haionyeshi dalili. Lakini wakati mwingine watoto wanapata:
Bega moja kuwa juu kuliko lingine
Nyonga moja kuwa juu kuliko nyingine na kusababisha kiuno kisichosambamba
Maumivu madogo hadi makali ya mgongo
Skoliosisi kali inaweza kusababisha:
Maumivu ya mara kwa mara
Ugumu wa kupumua, iwapo mbavu zinaweka shinikizo kwenye mapafu
Kuharibika kwa viungo vya ndani
Madaktari wanawezaje kujua kama mtoto wangu ana skoliosisi?
Daktari atamwomba mtoto wako ainame upande wa mbele ili kuona ikiwa uti wa mgongo umepinda
Ikiwa uti wa mgongo wa mtoto wako unaonekana kama unapinda, daktari wako atachukua eksirei za kuthibitisha skoliosisi.
Eksirei humsaidia daktari wako kutathmini kiwango cha upinde huo
Madaktari hutibu skoliosisi vipi?
Matibabu hutegemea kiwango cha upinde
Upinde mdogo unaweza usihitaji matibabu. Lakini madaktari watauchunguza mara kwa mara ili kuona ikiwa unazidi kuwa mbaya.
Katika hali mbaya zaidi, matibabu yanapaswa kuanza mapema iwezekanavyo na yanaweza kujumuisha:
Kiegemezi cha kusaidia kuweka sawa uti wa mgongo
Tiba ya kimwili ili kuzuia skoliosisi isizidi
Upasuaji wa kuunganisha mifupa ya uti wa mgongo
Mtoto wako anaweza kujisikia vibaya kuhusu kuwa na skoliosisi au kutopendezwa na matibabu. Kuzungumza na mshauri wa kitaalamu kunaweza kumsaidia mtoto wako kujisikia vizuri.