Muhtasari wa Maambukizi ya Njia ya Hewa Yanayosababishwa na Virusi kwa Watoto

NaBrenda L. Tesini, MD, University of Rochester School of Medicine and Dentistry
Imekaguliwa naBrenda L. Tesini, MD, University of Rochester School of Medicine and Dentistry
Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2023 | Imebadilishwa Apr 2025
v819247_sw

Maambukizi ya virusi kwenye njia ya upumuaji huathiri pua, koo, na njia za hewa na yanaweza kusababishwa na virusi mbalimbali.

  • Maambukizi ya kawaida ya njia ya upumuaji ni pamoja na mafua ya kawaida na homa ya mafua (influenza).

  • Dalili za kawaida ni pamoja na pua kuziba, mafua, koo kukwaruza, kikohozi, na mtoto kuwa na mahangaiko.

  • Utambuzi unategemea dalili.

  • Matibabu yanalenga kupunguza makali ya dalili.

  • Usafi mzuri ndiyo njia bora ya kuzuia maambukizi haya, na chanjo za kila mwaka zinaweza kusaidia kuzuia homa ya mafua (influenza).

Watoto hupata wastani wa maambukizi sita ya virusi kwenye njia ya upumuaji kila mwaka.

Maambukizi ya virusi kwenye njia ya upumuaji kwa kawaida hugawanywa katika:

  • Maambukizi ya njia ya juu ya upumuaji: Dalili hutokea zaidi kwenye pua na koo. Maambukizi haya ya njia ya juu yanaweza kutokea katika umri wowote na yanajumuisha mafua ya kawaida na homa ya mafua (influenza).

  • Maambukizi ya njia ya chini ya upumuaji: Dalili hutokea kwenye koo la hewa, njia za hewa, na mapafu. Maambukizi haya ya njia ya chini ni ya kawaida zaidi kwa watoto na yanajumuisha kikohozi cha kubweka (croup), bronchiolitis, na nimonia.

Wakati mwingine watoto hupata maambukizi yanayohusisha njia zote mbili za upumuaji, ya juu na ya chini.

Je, Ulijua...

  • Kupatwa na baridi, kulowana, au kuchoka hakusababishi mafua wala kumfanya mtoto awe na uwezekano mkubwa wa kuambukizwa.

Sababu za Maambukizi ya Virusi ya Upumuaji

Aina nyingi tofauti za virusi huambukiza njia ya upumuaji. Kwa watoto, virusi vya rhinovirus, virusi vya homa ya mafua (wakati wa mlipuko wa kila mwaka wa msimu wa baridi), virusi vya parainfluenza, virusi vya RSV (respiratory syncytial virus), enteroviruses, coronaviruses, na aina fulani za adenovirus ndizo sababu kuu.

Mara nyingi, maambukizi haya huenea pale mikono ya watoto inapogusana na majimaji ya puani kutoka kwa mtu aliyeambukizwa. Majimaji haya yana virusi. Watoto wanapojigusa pua au macho, virusi huingia mwilini na kuanzisha maambukizi mapya. Kwa nadra zaidi, maambukizi huenea pale watoto wanapovuta hewa yenye matone yaliyotolewa kwa kikohozi au chafya kutoka kwa mtu aliyeambukizwa.

Kwa sababu mbalimbali, majimaji ya puani au ya kupumua kutoka kwa watoto yana virusi vingi zaidi kuliko yale ya watu wazima. Kiasi hiki kikubwa cha virusi, pamoja na kukosa umakini kwenye usafi, huwafanya watoto wawe na uwezekano mkubwa wa kuambukiza wengine. Uwezekano wa kuambukizwa huongezeka zaidi pale watoto wengi wanapokusanyika pamoja, kama vile shuleni au kwenye vituo vya kulelea watoto. Kinyume na mawazo ya watu wengi, mambo kama kupatwa na baridi, kulowana na mvua, au kuchoka hayasababishi mafua wala kuongeza hatari ya mtoto kuambukizwa.

Dalili za Maambukizi ya Virusi ya Upumuaji

Virusi vinapovamia seli za njia ya upumuaji, husababisha uvimbe na kutoa kamasi nyingi. Hali hiki husababisha pua kuziba, mafua, koo kuwasha, na kikohozi ambacho kinaweza kudumu hadi siku 14. Baadhi ya watoto wanaweza kuendelea kukohoa kwa wiki kadhaa hata baada ya maambukizi ya juu kuisha. Homa ya kufikia nyuzi joto 101 hadi 102 F (takribani 38.3 hadi 38.9 C) ni kawaida kwa watoto wadogo au wale wenye homa ya mafua (influenza). Joto la mtoto linaweza hata kupanda hadi kufikia 104 F (40 C).

Dalili nyingine za kawaida kwa watoto ni pamoja na kukosa hamu ya kula, uvivu/uchovu, na kujisikia mgonjwa kwa ujumla. Maumivu ya kichwa na mwili hujitokeza, hasa kukiwa na homa ya mafua. Watoto wachanga na wadogo hawawezi kuelezea dalili zao, hivyo huonekana tu kuwa na kero na kutotulia.

Matatizo ya maambukizi ya virusi ya njia ya upumuaji kwa watoto

Kwa sababu watoto wachanga hupendelea kupumua kupitia pua, hata kuziba kidogo kwa pua kunaweza kuwasababishia ugumu mkubwa wa kupumua. Pua kuziba pia husababisha matatizo wakati wa kunyonya, kwani watoto hawawezi kupumua huku wananyonya titi au chupa. Kwa kuwa hawawezi kutema kikohozi, mara nyingi hupatwa na kichefuchefu au kusongwa na kamasi.

Njia ndogo za hewa za watoto wadogo zinaweza kuziba sana kutokana na uvimbe na kamasi, jambo linalofanya upumuaji kuwa mgumu. Watoto hupumua kwa kasi na wanaweza kutoa sauti nyembamba wakati wa kutoa pumzi (wheezing) au sauti inayofanana na hiyo wakati wa kuvuta pumzi (stridor). Kuziba sana kwa njia ya hewa kunaweza kumfanya mtoto apumue kwa taabu na kubadilika rangi na kuwa wa bluu (cyanosis). Matatizo hayo ya njia ya hewa hutokea zaidi kukiwa na maambukizi ya virusi vya parainfluenza, RSV, na human metapneumovirus. Watoto wanaopumua kwa taabu au wenye rangi ya bluu (cyanosis) wanahitaji kuonwa na daktari kwa dharura.

Baadhi ya watoto wenye maambukizi haya pia hupata maambukizi ya sikio la kati (otitis media) au ya tishu za mapafu (nimonia). Maambukizi haya yanaweza kusababishwa na virusi vyenyewe au na bakteria wanaoshambulia kwa sababu uvimbe wa virusi umedhoofisha tishu. Kwa watoto wenye pumu, maambukizi ya njia ya upumuaji mara nyingi huchochea shambulio la pumu.

Utambuzi wa Maambukizi ya Virusi ya Upumuaji

  • Tathmini ya daktari

Madaktari na wazazi hutambua maambukizi haya kupitia dalili za kawaida. Kwa ujumla, watoto wenye afya wanaopata dalili nyepesi za njia ya juu hawahitaji kumuona daktari, isipokuwa kama wanapata shida kupumua, hawawezi kunywa maji, au wana homa kwa zaidi ya siku mbili.

Picha za eksirei za shingo na kifua zinaweza kuchukuliwa kwa watoto wenye shida ya kupumua, sauti ya stridor, au kutoa sauti ya kukwama kwa pumzi (wheezing).

Vipimo vya damu na vya majimaji ya njia ya upumuaji mara nyingi havihitajiki.

Matibabu ya Maambukizi ya Virusi ya Upumuaji

  • Pumziko na unywaji wa maji mengi

  • Dawa za kupunguza homa na maumivu

Antibiotiki hazitolewi kwa sababu haziwezi kuua virusi vya njia ya upumuaji.

Watoto wenye maambukizi haya wanahitaji kupumzika zaidi na kunywa vinywaji vya kutosha. Acetaminophen au dawa ya kupunguza uvimbe isiyo na asteroidi (NSAIDs), kama vile ibuprofen, zinaweza kutolewa kwa homa na maumivu.

Kwa watoto wachanga, pua kuziba kunaweza kupunguzwa kwa kutumia kifaa cha kunyunyizia hewa (cool-mist vaporizer) na kwa kufyonza kamasi kwa kutumia raba maalum (suction bulb).

Kuna dawa za kuzuia virusi vya homa ya mafua (influenza) zinazoweza kutumiwa na watoto. Hata hivyo, dawa hizi hufanya kazi tu zikitumika ndani ya siku mbili za kwanza tangu dalili kuanza, na hufupisha muda wa kuugua kwa takribani siku moja tu.

Watoto wakubwa wanaweza kutumia dawa za kuzibua pua (decongestants) zinazouzwa madukani, ingawa mara nyingi hazisaidii sana. Watoto wachanga na wadogo wanaweza kupata madhara mabaya kutokana na dawa za kuzibua pua kama vile mahangaiko, kuchanganyikiwa, na mapigo ya moyo kwenda mbio, hivyo hawapaswi kupewa kabisa.

Kinga ya Maambukizi ya Virusi ya Upumuaji

  • Usafi mzuri

  • Chanjo dhidi ya homa ya mafua

Hatua bora ya kuzuia ni kufanya usafi mzuri. Mtoto mgonjwa na watu wa nyumbani wanapaswa kunawa mikono mara kwa mara. Kwa jumla, kadri mgusano wa kimwili (kama vile kukumbatiana, au kushiriki kitanda) unavyofanyika na mtoto mgonjwa, ndivyo hatari ya kueneza maambukizi kwa wanafamilia wengine inavyoongezeka. Lazima wazazi wasawazishe hatari hii na hitaji la kumfariji mtoto mgonjwa. Watoto wanapaswa kubaki nyumbani na wasiende shule hadi homa itakapokwisha na wajisikie wenye nguvu za kutosha.

Homa ya mafua na COVID-19 zinaweza kuzuiwa kwa chanjo. Watu wote kuanzia umri wa miezi 6 wanapaswa kupata chanjo ya influenza kila mwaka (tazama pia Chanjo ya Homa ya Mafua). Watu wote wenye umri wa miezi 6 na zaidi wanapaswa kuwa wamepata chanjo ya COVID-19 ya hivi karibuni kulingana na ratiba za chanjo za sasa (tazama pia Maelekezo ya CDC ya Muda ya Kimatibabu kwa Matumizi ya Chanjo za COVID-19 Yaliyopitishwa au Kuruhusiwa nchini Marekani). Chanjo ni muhimu hasa kwa wale wenye matatizo ya moyo, mapafu (pamoja na pumu), kisukari, au ugonjwa wa seli mundu. Pia, watoto wenye mfumo dhaifu wa kinga, kama wale wenye VVU au wanaopata matibabu ya kansa (chemotherapy), wanapaswa kuchanjwa.

Taarifa Zaidi

Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa MIONGOZO haiwajibikii maudhui kwenye rasilimali hii.

  1. Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC): Maelekezo ya Muda ya Kimatibabu kwa Matumizi ya Chanjo za COVID-19 nchini Marekani: Rejea inayotoa taarifa kuhusu chanjo zinazotumika Marekani, zikiwemo dozi na maelekezo kwa makundi yote ya umri na watu wenye mahitaji maalum.